Ruto ainua mikono

Ruto ainua mikono

Na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto jana aliinua mikono kuhusu nafasi yake serikalini akisema anayopitia yamepita mipaka.

“Hata kama dhahabu huwa inapitishwa motoni ili kuwa bora, nadhani changamoto zinazonikumba zimepita kipimo,” akasema Dkt Ruto jana kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Inooro FM.

Aliwalaumu Rais Uhuru Kenyatta, Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na waliokuwa vinara wa NASA kwa kumsukuma kwenye kona, hali ambayo imemuacha bila mamlaka yoyote serikalini.

Dkt Ruto alisema tangu 2018, Rais Kenyatta alipomkumbatia Kiongozi wa ODM Raila Odinga, amekuwa mtazamaji tu, ilhali waliokuwa wapinzani wa Jubilee ndio sasa wanaendesha masuala ya serikali.

“Wakati muhula wa pili ulipoanza, niliambiwa nikae kando. Majukumu yangu yalikabidhiwa Dkt Matiang’i na niliheshimu uamuzi wa Rais Kenyatta kama bosi wangu.”

Kauli yake ilijiri siku mbili baada ya kuzuiwa kusafiri nchini Uganda Jumatatu kwa ziara ya kibinafsi katika hali tatanishi, hatua aliyotaja kuwa njama za makusudi ya kumpiganisha na Rais Kenyatta.

Akirejelea kiini cha tofauti zake na Rais Kenyatta, Dkt Ruto aliwalaumu viongozi wa uliokuwa muungano wa Nasa – Bw Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) kwa masaibu ambayo yamekuwa yakiukumba utawala wa Jubilee.Alisema wanne hao ndio “walivamia” Jubilee na “kumwelekeza Rais Kenyatta kusiko,” hali ambayo alisema imeleta mchanganyiko uliopo kwa sasa.

“Tulipoanza kuhudumu katika muhula wa pili, tulikita mipango yetu ya kiuchumi kwenye Ajenda Nne Kuu za Maendeleo. Hata hivyo, Nasa ilivuruga mipango hiyo yote.

“Badala ya kuangazia mipango hiyo, tulianza mambo ya handisheki na BBI. Kwa sasa, Jubilee imevurugika, Nasa imekufa na mipango yetu ya kiuchumi haipo tena,” akasema Naibu Rais.

Alisema Rais Kenyatta aliwaalika wanne hao kama marafiki kumsaidia kuendesha serikali, lakini badala yake walimpotosha kwa kumletea ajenda na mipango ambayo haiwiani hata kidogo na manifesto ya Jubilee.

Dkt Ruto alijitenga na masaibu yanayoikumba nchi, akisema alifanya kila alichohitajika kufanya kuokoa merikebu ya Jubilee isizame.

“Wakenya wamekuwa wakiniuliza hatua nilizochukua kuisaidia serikali ya Jubilee. Mchango wangu uko katika miradi muhimu ya maendeleo tuliyozindua na kutekeleza katika muhula wa kwanza kama Reli ya Kisasa (SGR), usambazaji umeme nchini na ujenzi wa barabara. Nimetengwa katika muhula wa pili,” akasema.

Alijipigia debe kama mwaniaji urais bora zaidi 2022, aliye na suluhisho kwa changamoto za kiuchumi zinazoikumba nchi kwa sasa.

Alisema licha ya kuwa katika serikali iliyowavunja moyo Wakenya, ana uwezo wa kubadilisha uchumi kama alivyofanya Rais Mstaafu Mwai.

“Wakenya huwa wanamsifia Bw Kibaki kwa kazi aliyofanya kama Rais wala si yale aliyoyafanya alipohudumu kama makamu wa rais katika serikali ya marehemu Daniel Moi. Vivyo hivyo, ningetaka wanikumbuke kwa yale nitakayowafanyia kama rais wao ikiwa watanichagua mwaka ujao,” akasema.

Licha ya hayo, baadhi ya washirika wa Rais Kenyatta walitaja kauli za Dkt Ruto kama hadaa kwa Wakenya, ikizingatiwa amekuwa serikalini tangu 2013.

Kulingana na mbunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Dkt Ruto ni kama dereva anayemlaumu mwenzake wakati gari lao linapopata ajali.

“Dkt Ruto kamwe hawezi kujitenga na changamoto zinazoikumba nchi au ahadi ambazo hazijatimizwa hadi sasa. Yeye ni sehemu ya serikali hii,” akasema.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tumekisaliti kizazi cha sasa kwa jina la...

Mfanyabiashara anayeshtakiwa kujaribu kuua maafisa wawili...