Habari Mseto

Ruto ajikumbusha maisha ya 'uhasla'

April 22nd, 2018 1 min read

DPPS na BERNARDINE  MUTANU

NAIBU Rais William Ruto Jumamosi alijikumbusha siku za kuwa ‘hasla’ kwa kutembelea Kambi Kuku mjini Eldoret, Uasin Gishu.

Akiwa kijana, Bw Ruto alikuwa mfanyabiashara katika soko hilo akiwauzia kuku waendeshaji magari.

Alifika sokoni humo kuzindua mnada wa kuku, ambao ni mradi wa kipekee nchini.

Kila hadithi maishani ina mwanzo na thamani ya hadithi ni umbali aliofika mtu kutoka mwanzoni. Tofauti hiyo ndio watu hutumia kuelezea ufanisi maishani. Kwa Bw Ruto, mwanzo haukuwa mwema.

Angeamka asubuhi na kwenda sokoni humo kuuzia waendeshaji magari kuku katika soko hilo ambalo halikuwa la kudumu katika barabara ya Eldoret kuelekea Malava.

Jumamosi, kiongozi huyo alizuru eneo hilo, ambako alitangamana na wauzaji wa kuku na kusikiliza hadithi zao kabla ya kuzindua mnanda wa kuku kwa lengo la kuuza kuku wao kwa bei bora.

Bw Ruto alisema uzinduzi wa mnada eneo hilo ambako alipata jina ‘hustler’ ilikuwa ni njia ya kuimarisha biashara miongoni mwa vijana na makundi ya kina mama.

Mnanda huo ulichangisha Sh6 milioni kwa kuwaleta wafugaji wa kuku wadogo kutoka Jua Kali, Turbo na maeneo yaliyo karibu pamoja ambapo kuku 5,000 waliuzwa, kila mmoja kwa Sh1, 200.

Akihutubia wafanyibiashara, Bw Ruto alisema serikali ya kaunti itasaidia wafugaji wa kuku eneo hilo kuunda chama cha ushirika.

Aliandamana na wabunge na viongozi wengine akiwemo Waziri wa Kawi Charles Keter na Seneta Kipchumba Murkomen.

Aliwashauri wakazi kuwekeza katika ufugaji wa kuku ili kuimarisha maisha yao na kuongeza kuwa ufugaji wa kuku ilikuwa nafasi nzuri ya wanawake na vijana kujiimarisha kimapato na kuondokea umaskini.