Habari MsetoSiasa

Ruto ajinadi kwa miradi Uhuru akikwama Ikulu

June 18th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto kwa wiki moja sasa ameonekana kuanza kujitokeza tena kuendeleza mtindo wa kupokea makundi ya wageni nyumbani kwake Karen, Nairobi baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu.

Alhamisi, Dkt Ruto alipokea makundi ya vijana ambao aliwapa ufadhili wa vifaa vya mamilioni ya pesa kuinua biashara zao.

Kinaya ni jinsi mikutano hii inafanywa wakati ambapo ilifichuka Rais Uhuru Kenyatta amesitisha mikutano ya Ikuluni kwa muda, baada ya watu wanne kupatikana wana virusi vya corona katika Ikulu hiyo ya Nairobi hivi majuzi.

Mnamo Jumatano, Kiongozi wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka alifichua kuwa Rais Kenyatta hangeweza kukutana na watu kwa sasa kutokana na maambukizi ambayo yalithibitishwa Ikulu.

Akihutubia vijana jana, Dkt Ruto alisema ameanzisha mpango wa kusaidia makundi ya vijana kujikimu kimaisha wakati huu ambapo biashara nyingi ndogo zimeathirika kwa janga la corona.

Kulingana naye, atakuwa akitoa misaada kwa makundi tofauti kila wiki kwa mwezi mzima hadi afikie takriban vijana 5,000 jijini Nairobi.

Vifaa alivyotoa jana vilijumuisha mashine za kuosha magari, tenki za maji, pikipiki na vyakula vya mifugo kama vile kuku na nguruwe.

“Serikali haiwezi kusaidia kila mtu. Itafikia sehemu kubwa lakini hilo halimaanishi mashirika na watu wengine wenye nia njema hawawezi kuchangia kusaidia Wakenya. Mimi na marafiki pamoja na wahisani pia tuliona tuchangie kusaidia wananchi. Hii ni awamu ya kwanza,” akasema.

Kwa kipindi cha wiki moja sasa, Dkt Ruto amekutana pia na viongozi wa kidini, wandani wake wa kisiasa kutoka eneo la Magharibi, na makundi ya wanawake kutoka jamii ya Waislamu.

Kabla hapo, alikuwa ametuliza mikutano aina hiyo wandani wake wakasema alikuwa akijihusisha kutoa misaada kwa jamii zinazokumbwa na makali ya janga la corona ‘chini ya maji’.

Kimya chake kilitokea wakati ambapo wandani wake katika Bunge la Taifa na Seneti walikuwa wakiangukiwa na shoka la Jubilee, wakitimuliwa katika nafasi za uongozi bungeni.

Licha ya kuanza kujitokeza, Naibu Rais jana alikataa kujadili siasa.

“Wakati wa siasa haujafika. Sasa ni wakati wa kutafuta riziki. Kila mtu ashughulikie kujisaidia. Siasa itakuwa na wakati wake na tutanyoroshana wakati huo ukifika. Saa hizi tujipange ili tuhakikishe kila mmoja anafikia malengo yake ya kimaisha,” akaambia vijana waliokuwepo.

Alikuwa ameandamana na Wabunge John Kiarie (Dagoretti), James Gakuya (Embakasi Kaskazini) na Nixon Korir (Langata).

Katika hotuba zao, wabunge hao waliashiria kwamba misaada iliyotolewa kwa vijana ni sehemu ya mikakati ya kisiasa ya Dkt Ruto anapojiandaa kwa kinyang’anyiro cha kumrithi Rais Kenyatta ifikapo mwaka wa 2022.

“Mtu anayekukumbuka wakati kama huu ndiye rafiki wa dhati. Wakati wake ukifika akituhitaji, kuna mtu atasema kingine kando na kwamba tumrudishie mkono?” akauliza Bw Gakuya.

Bw Korir alisema mpango uliopo ni kufikia makundi yote ya vijana Nairobi, huku Bw Kiarie akisema mpango huo utapanuliwa kujumuisha pia usaidizi kwa makundi ya kina mama.