Habari

Ruto ajipa raha ngoma ya BBI ikitulia moto

November 23rd, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto anaendelea kujivinjari jijini Dubai, Milki za Kiarabu, huku Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wakisalia kimya kuhusu hatima ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Naibu wa Rais jana alichapisha video katika mitandao ya kijamii ambapo alionekana akitafuna vinono katika moja ya migahawa kifahari jijini Dubai.

Katika video hiyo, Dkt Ruto, ambaye ameandamana na aliyekuwa Seneta wa Mombasa Omar Hassan, anaonekana akikatiwa nyama na mpishi maarufu Nusrek Gokche anayetamba kote duniani kwa jina la “Salt Bae’.

Dkt Ruto alisema kuwa Gokche, raia wa Uturiki aliyejizolea umaarufu kutokana na uuzaji wa nyama, ni mlalahoi aliyefanikiwa kibiashara kutokana na weledi wake wa kumimina chumvi kwenye kitoweo.

“Leo jioni nilitangamana na Salt Bae, mlala hoi Mturuki anayefanya kazi ya kuuza nyama ambaye alifanikiwa maishani kwa nyama, kisu na chumvi.

“Walalahoi katika masoko ya Kenyatta, Burma, Dagoreti na wengineo mmepata ushindani na mnaweza kujifunza mengi kutoka kwake. Kazi ni kazi,” akasema Dkt Ruto baada ya kusutwa mitandaoni kwa kutafuna mapochopocho huku Wakenya walala hoi ambao amekuwa ‘akiwatetea’ wakihangaika.

Baadhi ya Wakenya walishutumu naibu rais kwa kumtaja Salt Bae kama mlalahoi ilhali anamiliki hoteli kadhaa za kifahari. Kulingana na wakosoaji wake, Salt Bae ni bilionea ambaye hafai kulinganishwa na Wakenya walalahoi wanaohangaika kupata chakula.

Licha ya kuweka wazi kwamba yuko ziarani Dubai, Dkt Ruto hajafichua lengo la ziara hiyo katika Milki za Uarabuni (UAE).

Dkt Ruto, alielekea Dubai mnamo Jumatano baada ya kuahirishwa kwa uzinduzi wa shughuli ya kukusanya saini ili kuanza mchakato wa kurekebisha Katiba kupitia BBI.

Rais Kenyatta alifaa kuzindua shughuli hiyo Alhamisi wiki iliyopita. Kulingana na ripoti, Dkt Ruto alikutana na Rais Kenyatta kujadili BBI kabla ya kuelekea Dubai.

Ofisi ya BBI, inayoongozwa na aliyekuwa mbunge wa Dagoretti Kusini Dennis Waweru na mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed Jumatano, ilisema kuwa waliahirisha uzinduzi wa zoezi hilo sababu walichelewa kuchapisha Mswada wa Kurekebisha Katiba wa 2020. Wawili hao walisema kuwa watatangaza tarehe mpya ya uzinduzi huo.

Baada ya kuahirishwa kwa shughuli hiyo, Bw Odinga aliondoka nchini kimyakimya na kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo alikutana na Rais Felix Tshisekedi pamoja na gavana wa Lualaba, Richard Muyej, na mwenzake wa Haut- Katanga, Jacques Kyabula.

Bw Odinga alisema kuwa alienda DRC kama Mkuu wa Miundomsingi wa Umoja wa Afrika (AU) kukagua shughuli ya ujenzi wa mradi wa umeme wa Inga.

Wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakitoa taarifa za kukinzana kuhusu kilichosababisha kuahirishwa kwa shughuli ya kukusanya saini.

Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya akizungumza Jumamosi katika hafla ya mazishi alisema kuwa waliahirisha mchakato huo ili kutoa fursa ya kurekebisha makosa kwenye mswada wa BBI.

“Watu wanasema eti BBI imezimwa; huo ni upuuzi. Tulisitisha sababu kulikuwa na marekebisho madogo,” alieleza.

Akaongeza: “BBI ni nzuri asilimia 75. Mtoto akipata 75 kwenye mtihani anapata alama A; basi tuendelee mbele. Magavana wa Nyanza na Magharibi tulikutana wiki iliyopita jijini Kisumu pamoja na wataalamu, na tukapata mambo machache ambayo tunataka yarekebishwe na kisha tuendelee mbele.”

Naye Bw Waweru Jumamosi alisema kuwa fomu itakayotumika kukusanya saini haikuwa imeidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Kumekuwa na madai mengi kwenye mitandao ya kijamii lakini nataka kuwahakikishia Wakenya kwamba meli ya BBI tayari imeng’oa nanga na haitasimama,” akasema Bw Waweru.