Ruto ajipatia njia kukwepa kosa la Uhuru

Ruto ajipatia njia kukwepa kosa la Uhuru

NA ONYANGO K’ONYANGO

RAIS William Ruto ameamua kusimamia masuala ya muungano wa Kenya Kwanza (KKA) kutumia mbinu ya mashauriano hali ambayo imemfanya kupata uungwaji mkono kutoka kwa wabunge.

Tofauti na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, ambaye wabunge walilalama kuwa ilikuwa vigumu kwao kumfikia, Rais Ruto aliamua kufungua milango yake kwa viongozi wote katika muungano wa KKA.

Tangu aingie afisini Septemba 13, Rais Ruto ameitisha mikutano minne ya kundi la wabunge wa muungano huo, ambako inadaiwa huwa anawapa wabunge nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu maamuzi yaliyochukuliwa na serikali.

Ikiwa kuna suala kuu ambalo wabunge wanahitaji kutoa maamuzi, kabla ya lifanyike, Rais Ruto huitisha mkutano kulijadili.

Taifa Leo imegundua kuwa kila siku nyakati za jioni Rais Ruto huwapigia simu wabunge kadhaa wa KKA akiwauliza kuhusu shida wanazokumbana nazo katika maeneo bunge yao na jinsi serikali inaweza kuingilia kati kuzitatua.

Rais Ruto anaonekana kupata funzo kutoka kwa mtangulizi wake ambaye kutofikiwa kwake na wabunge kulichangia umaarufu wake kudorora katika Mlima Kenya ambako viongozi wakiongozwa Naibu Rais Rigathi Gachagua waliamua kumuasi.

Viongozi wengine kutoka Mlima Kenya walioongoza uasi dhidi ya Bw Kenyatta ni; Waziri wa Biashara Moses Kuria (wakati huo akiwa mbunge wa Gatundu Kusini), Kiongozi wa wengi Kimani Ichungwa, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, miongoni mwa wengine, waliomlaumu kwa kukumbatia uongozi wa kidikteta.

Jana Jumatano, Mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama aliambia Taifa Leo kwamba uhusiano kati ya Serikali Kuu ma Bunge unapasa kuwa mzuri kwa sababu wajibu wao mkuu ni kuwafanyia kazi Wakenya.

“Hii ndio maana wakati huu kuna uhusiano mzuri kati ya Rais Ruto na wabunge,” Bw Muthama akasema.

Anasema kuwa hatua ya Rais Ruto kukutana na wabunge kila mara inampa nafasi ya kuelewa na hata kushughulikia changamoto zilizoko katika maeneo bunge yao.

“Mitindo ya uongozi huwa sio sawa. Kuna viongozi ambao huja na kufanya mabadiliko makubwa. Katika muhula wa kwanza wa utawala wa Uhuru kulikuwa na mikutano mingi ya PG hadi pale alipoamua kumtenda naibu wake na mikutano hiyo ikakatika. Sasa amerejelea kile ambacho alikuwa akifanya.” Bw Muthama akasema .

Mwenyekiti huyo wa UDA alieleza kuwa mikutano ya kila mara ambayo Rais Ruto anafanya na wabunge wa muungano wa KKA inalenga kumpa nafasi ya kuelewa mahitaji yao na yale ya wakazi wa maeneo bunge wanakowakilisha.

Kwa upande wake Mbunge wa Belgut Nelson Koech anasema mikutano ya kila mara ya PG inalenga kumaliza mwenendo wa ubinafsishaji wa siasa nchini.

“Katika manifesto ya Kenya Kwanza, Rais Ruto alitoa sababu tatu zilizomfanya kuwania urais; kutetea Katiba, kusafisha siasa zetu na kuzalisha nafasi za kazi. Kwa kuitisha PGs za kila mara Rais anatimiza ahadi yake ya kuleta ungwana katika siasa. Kwa hakika aliahidi kukomesha utamaduni wa kutumia mamlaka kuendeleza siasa za ubinafsi na kupalilia demokrasia inayoheshimu Katiba,” Bw Koech anasema.

  • Tags

You can share this post!

Soka: Fahamu jinsi Kinale Girls inavyojiandaa kwa ajili ya...

Kura ‘ziliuzwa’ kwa Sh600, shahidi adai

T L