Habari za Kitaifa

Ruto akaa ngumu kuhusu ushuru wa nyumba

January 26th, 2024 1 min read

GITONGA MARETE Na KALUME KAZUNGU

RAIS William Ruto amesisitiza Ijumaa kwamba serikali ya Kenya Kwanza itaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu licha ya Mahakama ya Rufaa kukataa kurefusha agizo la kuruhusu serikali kuendelea kukata ushuru wa ujenzi wa nyumba hizo.

Kiongozi wa nchi akihutubu katika eneo la Kiutine, Kaunti ya Meru, alisisitiza kwamba ana uungwaji mkono kutoka kwa idadi kubwa ya raia, mradi anaosema unabuni nafasi za ajira kwa maelfu ya Wakenya.

Rais Ruto alisema sauti ya wananchi ni sauti ya Mungu.

“Nyinyi ndio wa kusema Kenya hii. Kuna uhusishaji mwingine wa umma tofauti na huu wenu,” akauliza Rais Ruto ambapo ameahidi kuendeleza mbele miradi ya aina hiyo.

Alisema mahakama inafaa kuipa serikali muda inapoendelea kutunga sheria jinsi ilivyoagizwa.

“Tayari tunaendelea na mchakato wa kutunga sheria ya namna mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu utakavyofanikishwa,” ameongeza.

Rais amekuwa akizindua ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Tayari ameshazindua miradi hiyo katika kaunti za Nairobi, Uasin Gishu, Laikipia, Nyeri na Meru miongoni mwa kaunti nyingine.

Kamati ya Bunge kuhusu Masuala ya Ujenzi wa Nyumba za Bei nafuu mnamo Ijumaa ilizuru Lamu kukutana na umma kukusanya maoni yao kuhusu Mswada wa Nyumba za Bei Nafuu wa 2023.

Kamati hiyo ilianzia shughuli zake Faza, Lamu Mashariki kabla ya kuelekea kwa Ukumbi wa Umma ulioko mjini Mokowe, Lamu.

Mnamo Januari 22, 2024, kamati hiyo ilikuwa katika ukumbi wa Kaunti ya Uasin Gishu ulioko mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu. Kikao cha Eldoret kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha na Mipango ya Kitaifa Kimani Kuria.