HabariSiasa

Ruto akaa ngumu wabunge wakitaka afikishwe kortini

April 1st, 2019 2 min read

NDUNG’U GACHANE, WANDERI KAMAU Na DPPS

SIASA kuhusu Naibu Rais William Ruto, zilichacha Jumapili huku viongozi wanaompiga vita wakitaka ashtakiwe kwa madai ya ufisadi, na wanaomuunga mkono wakisisitiza haendi kokote.

Wapinzani wa Dkt Ruto, ambao walijumuisha wabunge wa vyama vya Jubilee, ODM, Wiper na Kanu, walikusanytika katika Kaunti ya Murang’a, ambapo walimwambia Rais Uhuru Kenyatta kukoma kuwatisha watu katika serikali yake wanaoshukiwa kuwa wafisadi, na badala yake awachukulie hatua kali hata kama ni naibu wake anayeshukiwa.

Wabunge hao waliozungumza katika eneo la Gatanga, walisema wakati wa vitisho umekwisha na Wakenya wanataka kuona wafisadi katika ngazi za juu serikalini wakipelekwa mahakamani.

Viongozi hao walijumuisha Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a), wabunge Nduati Ngugi (Gatanga), Gladys Wanga (Homa Bay), T. G. Kanjwang (Ruaraka), Gathoni Wamuchomba (Kiambu), Maina Kamanda (Kuteuliwa), Dr James Nyikal (Seme), Robert Mbui (Kathiani), Caleb Khamisi (Saboti), Maoka Maore (Igembe Kaskazini), William Kamket (Tiaty), Mercy Gakuya (Kasarani) na Joshua Kutuny (Cherangany).

Pia walikuwepo Beatrice Elachi (aliyekuwa spika wa Nairobi) na David Murathe (aliyekuwa naibu mwenyekiti wa Jubilee).

“Tumeshuhudia wakuu wa serikali katika nchi za kigeni wakikamatwa na hata kufungwa kwa ufisadi. Naibu Rais hayupo juu ya sheria, na kama amehusika kwenye ufisadi basi akamatwe na kushtakiwa,” akasema Bw Murathe.

Bw Mbui alimtaka Rais Kenyatta kuwataja maafisa wafisadi katika serikali yake wakati atakapohutubia Bunge hapo Alhamisi.

Katika Kaunti jirani ya Kiambu, wafuasi wa Dkt Ruto waliapa kuwa juhudi zozote za kumhujumu kinara wao hazitafua dafu.

Wanasiasa hao walikuwa ni magavana Ferdinand Waititu (Kiambu), Joseph Ole Lenku (Kajiado) na Moses Lenolkulal (Samburu).

Wabunge walikuwa Josphat Kabeabea (Tigania Mashariki), Alice Wahome (Kandara), Jayne Kihara (Naivasha), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Jude Jomo (Kiambu Mjini), Catherine Waruguru (Laikipia), Peris Tobiko (Kajiado Mashariki), George Sunkuiya (Kajiado Magharibi), Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Rindiki Mugambi (Buuri), Janet Teiya (Kajiado) na Didmus Barasa (Kimilili).

Walidai upinzani bado unapanga kumng’oa mamlakani Dkt Ruto.