Habari za Kitaifa

Rais Ruto amshukuru Biden kwa mlo mtamu, makaribisho mazuri

May 25th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amemmiminia shukrani Rais wa Amerika Joe Biden kwa mapokezi mazuri aliyompa na dhifa murua ya chajio aliyomwandalia Alhamisi jioni katika Ikulu ya White House, jijini Washington DC.

Kwenye taarifa Ijumaa Mei 24, 2024, Dkt Ruto alisema hafla hiyo ilikuwa yenye kumbukumbu kubwa na kilele cha uhusiano wa miaka 60 kati ya Amerika na Kenya.

“Kwa niaba yangu na ujumbe wangu, namshukuru Rais Joe Biden na Mama Taifa Jill Biden kwa mapokezi yenu na dhifa ya kitaifa ya chakula cha jioni. Mapokezi yenu mazuri yalifanya usiku huo kuwa wa kukumbukwa na ninashukuru. Asante Rais,” Rais Ruto akasema Ijumaa kwenye taarifa kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.

Rais Ruto aliondoka nchini Kenya mnamo Jumapili jioni kwa ziara kwa mwaliko wa Rais Biden, ziara iliyofikia kikomo Ijumaa.

Wakati wa ziara hiyo, kiongozi huyo wa taifa la Kenya alitia saini mikataba kadhaa kuhusu uwekezaji, ikiwemo ule wa thamani ya Sh23 bilioni na kampuni ya Coca-Cola.

Aidha, Amerika ilikubali kufadhili mradi wa upanuzi wa barabara kuu ya Nairobi-Mombasa ili iwe yenye safu nane, nne kila upande kwa gharama ya Sh471 bilioni huku wizara ya elimu ikipigwa jeki kwa msaada wa Sh4.7 bilioni.

Rais Biden alimhakikishia Ruto kwamba daima Amerika na Kenya zitasimama pamoja kwa lengo la kujiendeleza.

“Leo nina matumaini kama yale ambayo wazalendo wa Kenya walikuwa nayo walipopandisha bendera mpya juu usiku wa manane. Kenya na Amerika zinasimama pamoja. Zimejitolea kusaidiana. Zimejitolea kwa raia wao. Na zimejitolea kujenga ulimwengu mpya,” Rais Biden akasema kupitia taarifa kwenye mitandao ya kijamii.

Waziri wa Ulinzi wa Amerika Lloyd Austin alimuaga rasmi Rais Ruto ambaye baada ya hapo aliabiri ndege kurejea nchini.