Ruto akataa talaka ya Uhuru

Ruto akataa talaka ya Uhuru

VALENTINE OBARA na LUCY MKANYIKA

MAJIBIZANO makali yameibuka upya kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake, Dkt William Ruto huku rais akimshinikiza Dkt Ruto kuondoka serikalini.

Kwenye mahojiano katika Ikulu ya Nairobi, Jumatatu, Rais Kenyatta alilalamikia jinsi ambavyo Dkt Ruto amekuwa akikaidi misimamo ya serikali kuu tangu alipoamua (kiongozi wa nchi) kushirikiana na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kupitia ‘handisheki’ mnamo 2018.

Hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Rais kuhojiwa na wanahabari, tangu arejee mchini kutoka Uingereza Julai 30, na tangu Mahakama ya Juu idumishe uamuzi wa Mahakama Kuu na kuharamisha marekebisho ya Katiba kupitia kwa Mpango wa Maridhiano (BBI).

“Katika jamii watu wasipoelewana, jambo la heshima kiongozi anafaa kufanya ni kusema, “sikubaliani na sera za serikali hii kwa hivyo nataka kujitenga nayo”, kisha awasilishe barua ya kujiuzulu. Natamani sana watu wangekuwa wanafanya hivi. Huwezi kuishi ndani ya nyumba kisha uwe unaibomoa wakati huo huo,” akasema Rais Kenyatta.

Hata hivyo, Dkt Ruto, Jumanne alipuuzilia mbali wito wa kumtaka ajiuzulu na kusisitiza ataendelea kumenyana na wakosoaji wake akiwa serikalini.

Alikuwa akizungumza katika mazishi ya Ronald Habel Sagurani, ambaye alikuwa diwani wa Wadi ya Mahoo, Kaunti ya Taita Taveta hadi kifo chake wiki iliyopita.

“Kwa wale wanaoona nimewakosea, nawomba msamaha. Lakini nimeamua ya kwamba sina nafasi ya kurudi nyuma wala starehe ya kusalimu amri. Nawaomba wanielewe kuwa niko na kazi maalumu ya kutekeleza kwa sababu tumeamua tutabadilisha uchumi,” akasema.

Tangu 2018, Naibu Rais amekuwa akilalamika kuwa ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ulitatiza utekelezaji wa mipango ya serikali ya Jubilee kufanikisha maendeleo nchini, akidai muda na rasilimali nyingi za serikali zilitumiwa kwa kampeni za BBI.

Mivutano kati ya viongozi hao wawili wakuu serikalini ilifikia kiwango cha kuwa, Naibu Rais alionekana kama mwanaharamu asiyependwa nyumbani.

Licha ya kuwa baadhi ya majukumu yake yalikabidhiwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, huku pia mawaziri, makatibu wa wizara na Bw Odinga wakitumwa kumwakilisha Rais katika hafla mbalimbali, Rais Kenyatta alisisitiza huwa anashirikisha viongozi wote katika maamuzi yake.

“Nimejaribu kadri ya uwezo wangu kuhusisha kila mtu serikalini ikiwemo wale wanaoikosoa. Kama hupendezwi na ajenda yangu niliyochaguliwa kutekeleza, ondoka uachie wengine nafasi kisha wewe utapata nafasi yako baadaye utekeleze yako. Huwezi kutuambia huondoki na wakati huo huo hatuelewani, ni lazima uamue,” alisema Rais Kenyatta.

Kulingana na Dkt Ruto, mipango ya kurekebisha katiba ambayo iliharamishwa na Mahakama Kuu kisha katika Mahakama ya Rufaa wiki iliyopita, ilikuwa imelenga kuwanufaisha viongozi wachache na kumsaidia Bw Odinga kushinda urais kwa urahisi 2022.

Hata hivyo, Rais Kenyatta alipohojiwa Jumatatu alirejelea msimamo wake kuwa BBI ililenga kuleta mabadiliko ambayo yangemfaa raia wa kawaida, na hivyo basi maamuzi ya mahakama ni pigo kubwa kwa wananchi.

Alitoa mfano wa pendekezo la kuongeza idadi ya maeneobunge, ambapo, kulingana naye, lingepelekea maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu kugawanywa na hivyo basi ugavi wa fedha za Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF) kufanywa kwa njia ya usawa.

Rais alipuuzilia mbali kuwa BBI ilinuiwa kumwezesha Bw Odinga kuingia Ikulu, wala yeye mwenyewe kuongeza kipindi chake cha uongozi.

Lakini kama mwanandoa asiyetaka kujibizana na mwenzake ana kwa ana wanapozozana, Dkt Ruto alitumia fursa mazishini Taita Taveta kusisitiza msimamo wake kwamba BBI ilijali masilahi ya vigogo wa kisiasa.

Imani ya Naibu Rais na wandani wake kuhusu msimamo huu wa BBI imekuwa ikitiliwa nguvu katika siku za hivi majuzi, ambapo Rais aliandaa vikao mara mbili katika Ikulu ya Mombasa na Bw Odinga, pamoja na vinara wa Muungano wa OKA.

You can share this post!

Omondi na klabu yake ya Jonkopings waonja ushindi wa pili...

AKILIMALI: Kuku wa kienyeji wanampa donge nono