Ruto akatwa mbawa

Ruto akatwa mbawa

WANDERI KAMAU na CHARLES WASONGA

MASWALI yameibuka kuhusu ikiwa maafisa wakuu katika Afisi ya Naibu Rais William Ruto walikosa kuzingatia itifaki zote zinazohitajika ili kumruhusu kusafiri nje ya nchi baada ya Ruto kuzuiwa kusafiri Uganda, Jumatatu.

Kulingana na taratibu za kiserikali, Naibu Rais ni miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu zaidi serikalini ambao lazima wapate idhini ya Afisi ya Rais kabla kusafiri nje ya nchi.

Dkt Ruto alijipata katika njiapanda Jumatatu, alipocheleweshwa na hatimaye kuzuiwa kuelekea Uganda katika hali ya kutatanisha, baadhi ya maafisa katika Idara ya Uhamiaji wakisema kuna taratibu ambazo hazikuzingatiwa.

Dkt Ruto alilazimika kurejea katika makazi yake mtaani Karen, jijinii Nairobi, baada ya kucheleweshwa kwa karibu saa tano katika Uwanja wa Ndege wa Wilson.

Jana, washirika wake walitaja tukio hilo kama juhudi za muda mrefu zinazoendeshwa na maafisa wakuu serikalini kumhangaisha kisiasa.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo,’ mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) alitaja kisa hicho kama juhudi ambazo zimekuwa zikiendelea kuwatesa wanasiasa ambao wana uhusiano wa karibu na Dkt Ruto.

“Kama kawaida, watajaribu kugeuza ukweli wa mambo baada ya kubaini walifanya kosa la kisiasa. Walimzuia Naibu Rais kusafiri bila sababu yoyote. Sasa wanatafuta visingizio kwa kosa la kisiasa walilofanya,” akasema Bw Nyoro, akiwarejelea watu aliotaja kuwa “maafisa wakuu serikalini.”

Hata hivyo, kulingana na mbunge Jeremiah Kioni (Ndaragwa), ambaye mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC) na mshirika wa karibu wa Rais Uhuru Kenyatta, Dkt Ruto si kiongozi hivi hivi tu anayepaswa kufanya ziara za kibinafsi bila taratibu zifaazo kufuatwa.

“Kiongozi wa hadhi ya Naibu Rais ni kama mali ya nchi. Dkt Ruto aliacha kuishi maisha ya kibinafsi pindi alipochaguliwa kama Naibu Rais. Hivyo, lazima taratibu zote za kisheria zifuatwe kuhusu masuala muhimu kama kusafiri nje ya nchi,” akasema Bw Kioni.

Aliwalaumu maafisa wa afisi yake kwa kutozingatia taratibu za kisheria zinazohitajika ili kupata idhini inayohitajika kumruhsu kusafiri nje.Jana, mbunge Tom Kajwang (Ruaraka) alimtaka Naibu Spika Moses Cheboi kuwapa wabunge nafasi ya kujadili suala hilo, alilolitaja kama lenye uzito kitaifa.

Bw Kajwang’ alisema alitaka ufafanuzi ikiwa maafisa wa itifaki katika afisi ya Naibu Rais kwanza walitafuta idhini kutoka kwa Afisi ya Rais.

“Ninataka maelezo kuhusu ni kwa nini maafisa wa itifaki hawakufuata utaratibu ufao kwa kuomba idhini, hivyo kuaibisha Afisi ya Naibu Rais ambayo ni afisi ya kikatiba?” akauliza Bw Kajwang’.

“Kile kilichotokea jana katika Uwanja wa Wilson ambapo mshikilizi wa Afisi ya Naibu Rais alidhalilisha afisi hii ni muhimu. Kwa nini maafisa wa itifaki katika afisi hiyo waliruhusu kitendo kama hiki cha udhalilishaji kutokea hadharani?” akashangaa.

Hata hivyo, Bw Cheboi alikataa kusitisha shughuli za kawaida za Bunge kutoa nafasi kwa wabunge kujadili suala hilo, akisema Bw Kajwang hakufuata utaratibu ufaao.

“Bw Kajwang’ unafahamu fika kwamba kulingana na sheria za Bunge, ulifaa kuwasilisha ombi rasmi, kwa maandishi, kwa Afisi ya Spika ukiomba kusitishwa kwa shughuli za Bunge ili kutoa nafasi kwa mjadala kama huu kuendelea. Hata hivyo, nakubaliana nawe kwamba hili ni suala lenye uzito kitaifa,” akasema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na wabunge Dido Rasso (Saku) na Joseph Limo (Kipkelion Mashariki). Naye Mbunge Mwakilishi wa Kisii, Judithi Ong’era aliunga mkono kujadiliwa kwa suala hilo, bila kuwasilishwa kwa hoja maalum.

Wakati huo huo, washirika wa Dkt Ruto walikanusha madai kwamba, alisafiri jana nchini humo kwa kutumia njia za kibinafsi.Uvumi huo ulisambaa jana kwenye mitandao ya kijamii.

You can share this post!

Wazee wa Kaya mbioni kuunganisha Wapwani

Ndugu wawili wakana kuibia Benki ya Dubai Sh154milioni