Ruto akejeli muungano wa Uhuru na Raila

Ruto akejeli muungano wa Uhuru na Raila

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto amekejeli muungano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga huku akisema kuwa ajenda yao kuu ni kumzuia kuwa rais 2022.

Dkt Ruto ambaye jana alijitokeza wazi kupigia debe chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) alipohutubia wakazi wa maeneo ya Makutano, Akirimet na Kitalekabel, Kaunti ya Pokot Magharibi, alitaja muungano huo kuwa wa ‘viongozi wasiokuwa na maono.’

“Wanasiasa hao wanaungana kwa lengo la kumzuia William Ruto kuwa rais 2022 badala ya kuwaeleza Wakenya ajenda yao ya maendeleo,” akasema Naibu wa Rais.

Dkt Ruto alikejeli muungano huo siku moja baada ya chama cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Kenyatta kutangaza kuwa kitaungana na ODM chake Bw Odinga ili kushinda urais 2022.

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju Ijumaa alisema kuwa tayari vyama hivyo viwili vimeteua kamati ya wataalamu 14 ambao wataandaa mikakati na mkataba wa makubaliano baina ya vyama hivyo viwili.

Uamuzi wa kuunda muungano baina ya Jubilee na ODM ulifanywa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Bw Tuju alisema kuwa chama tawala kitaanza juhudi za kujiimarisha kwa kufungua ofisi katika maeneobunge yote 290 na kufanya uchaguzi wa viongozi wake.

Viongozi wengine wa Nasa; Bw Musalia Mudavadi (ANC), Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya) hawajahusishwa na mazungumzo hayo.

Mnamo Juni 2020, chama cha Wiper kinachoongozwa na Bw Musyoka kilitia saini mkataba wa maelewano na Jubilee ambapo vyama hivyo viwili viliafikiana kushirikiana 2022.

Chama cha Kanu na Chama cha Mashinani (CCM) chake aliyekuwa gavana wa Bomet Isack Ruto, pia vilitia saini mkataba wa maelewano na Jubilee. Bw Ruto anayemezea mate kiti cha ugavana wa Bomet, hata hivyo, alijiondoa mwezi mmoja baadaye na kutangaza kuwa ataunga mkono Naibu wa Rais 2022.

Bw Musyoka na Bw Mudavadi tayari wametangaza kuwa hawataunga mkono Bw Odinga iwapo ataungwa mkono na Rais Kenyatta kuwania urais mwaka ujao.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa Naibu wa Rais Ruto huenda akanufaika iwapo Rais Kenyatta na Bw Odinga watawatenga viongozi wengine wa NASA.

Profesa Medo Misama, mhadhiri wa siasa, anasema kuwa Dkt Ruto anafaa kunasa angalau vinara wawili NASA ili kuyumbisha mpango wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Majaribio ya Dkt Ruto kutaka kunasa Bw Musyoka au Bw Odinga yamegonga mwamba baada ya Rais Kenyatta kuingilia kati.

Naibu wa Rais sasa analenga Bw Mudavadi au Seneta wa Bungoma Wetang’ula.

Waziri wa zamani Musa Sirma, ambaye ni mwandani wa kiongozi wa Kanu, wiki iliyopita alishutumu Bw Mudavadi huku akidai kwamba amekuwa vikao vya siri na Naibu wa Rais William Ruto.

Jana, Naibu wa Rais alisema kuwa miungano hiyo ni ya kikabila na kuwataka Wakenya kujiepusha na viongozi ‘wanaotegemea miungano ya kikabila kushinda viti’.

You can share this post!

Kamati yaonya Knec kuhusu jengo lililokwama

NI NCHI YA UNAFIKI