Habari

Ruto akera ODM 'kumpa Raila kazi ya Uwaziri Mkuu UK'

May 30th, 2019 2 min read

PETER MBURU na COLLINS OMULO

CHAMA cha ODM kimekerwa na mzaha wa Naibu Rais, Dkt William Ruto kwamba kiongozi wao, Bw Raila Odinga anaweza kwenda kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza.

Naibu Rais jana aliibua ucheshi alipopendekeza kwa utani kwamba Bw Odinga anaweza kuchukua mahali pa Bi Theresa May ambaye alijiuzulu kuwa Waziri Mkuu wa UK, kwa vile Kenya haina tena wadhifa huo kikatiba.

Wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, viongozi wa ODM walimkashifu Dkt Ruto kwa kugeuza hafla ya maombi kuwa ukumbi wa kisiasa.

Bw Sifuna alitaja matamshi ya Dkt Ruto katika hafla hiyo kuwa yasiyofaa, akisema aligeuza hafla tulivu kuwa na “ukosefu wa uwazi na uaminifu.”

Alisema Bw Odinga hajaomba msaada wa Dkt Ruto kupata kazi, akimkumbusha kuwa Bw Odinga ndiye aliyempa kazi ya uwaziri wakati wa serikali ya muungano.

“Tunafahamu ni nani aliye na uwezo wa kumtafutia mwingine kazi baina yao wawili. Isitoshe, vijana ndio wanaohitaji ajira, ilhali Naibu Rais anajidai kila wakati kuwa ana uwezo wa kumpa Bw Odinga kazi,” akasema Bw Sifuna.

“Tutawaambia vijana kuwasilisha karatasi zao na kuziacha katika afisi ya Naibu Rais ili awatafutie kazi kwani hiyo ndiyo inafaa kuwa kazi yake,” akaongeza.

Naibu Rais alitoa pendekezo hilo baada ya mhutubu mkuu katika hafla hiyo, ambaye ni afisa kutoka bunge la juu Uingereza, Bw Michael Hasting kueleza kuhusu changamoto zinazokumba nchi yake kwa sasa kutokana na kujiuzulu kwa Bi May hivi majuzi.

Aliuliza ikiwa Kenya inaweza kuwa na Waziri Mkuu yeyote wa ziada aende akawasaidie kuongoza Uingereza. Aliposimama kuhutubu, Dkt Ruto alijibu kwamba hakuna waziri mkuu humu nchini, lakini kunaye mstaafu ambaye anaweza kutolewa.

“Kwa sababu umekuwa mzuri kwetu, umetuma ombi tuwape waziri mkuu. Tuna mmoja mstaafu hapa, na kwa kuwa katiba yetu iliondoa wadhifa huo, tukutumie wasifukazi wake,” akasema Dkt Ruto na kuzua kicheko.

Rais Uhuru Kenyatta naye, baadaye aliendeleza suala hilo na kusema hata yeye amejitolea kukabidhi Uingereza viongozi wengine zaidi, si mmoja tu, wanaomtatiza ili waende wakapewe wadhifa wa uwaziri mkuu huko.

“Nina watu kadhaa ambao ninaweza kukabidhi Uingereza angalau nipate amani kwa miaka mitatu ijayo,” Rais akasema kwa utani.

Bw Odinga hakuhudhuria hafla hiyo kwani yuko ziarani jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Dkt Ruto, aidha alitumia hafla hiyo kueleza hadhira kuhusu maisha yake ya utotoni ambapo alikuwa katika familia maskini, akieleza jinsi alivyoenda shuleni bila viatu, hadi mwishowe akakwea ngazi na kuwa naibu rais anayeongoza pamoja na mwana wa aliyekuwa rais wa kwanza wa taifa hili (Rais Uhuru).

Kulingana naye, hakuwahi kufikiria kwamba mtoto ambaye alitembea kwa miaka mingi bila viatu angewahi kuongoza pamoja na mtoto aliyekuwa akiishi ikuluni katika miaka hiyo.

Katika fursa hiyo, aliwajibu wale ambao wamekuwa wakimkosoa kwa kuchanga mamilioni ya pesa kwa makanisa pamoja na kulia kanisani, akisema ni kwa kukumbuka umaskini ambao Mungu alimwondolea ndiposa huona umuhimu wa kumshukuru.

Seneta wa Pokot Magharibi, Bw Samuel Poghisio naye alichekesha hadhira alipodai kuwa wakati fulani akiwa katika hafla nchini Sudan Kusini alizomewa kwa kukosa kuketi mahali palipokuwa pa wageni wazawa wa huko kwa kudhaniwa kuwa alikuwa raia wa nchi hiyo.

Rais Salva Kiir ambaye alikuwapo alimwambia seneta huyo, kwa utani, kuwa hilo lilitokana na jinsi anavyofanana na watu wa Sudan Kusini.