HabariSiasa

Ruto akubali kukoma kutangatanga kisiasa

August 4th, 2019 1 min read

Na NDUNGU GACHANE

NAIBU Rais William Ruto Jumapili alionekana kuanza kutii mwito wa Rais Uhuru Kenyatta wa kukomesha kampeni za mapema, alipowaambia wanasiasa wa Jubilee wakome kutangatanga wakipiga siasa.

Badala yake, Dkt Ruto alisema ataanzisha juhudi za kuunganisha mirengo pinzani ndani ya Jubilee ili Serikali iweze kuzingatia utekelezaji wa ahadi zake kwa Wakenya.

Akizungumza katika Kaunti ya Murang’a, Naibu Rais aliwataka wanasiasa ambao wamejigawanya katika makundi ya Tangatanga na Kieleweke kuungana na kusaidia serikali katika ajenda ya maendeleo.

Kundi la Tangatanga linajumuisha wanasiasa wanaounga mkono Dkt Ruto kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022, huku kundi la Kieleweke likipinga juhudi hizo.

“Ninataka tuelewane ili tutembee pamoja safari hii. Nawaomba Wakenya hasa wafuasi wa Jubilee tuachane na siasa ya mirengo na siasa ya ugomvi. Sisi sote ni kitu kimoja, kiongozi wetu ni mmoja na manifesto yetu ni moja. Tuungane tutekeleze yale mambo rais wetu aliwaahidi Wakenya,” akasema Dkt Ruto.

Mwezi uliopita, Rais Kenyatta, ambaye ni kiongozi wa Jubilee alikataa wito wa Dkt Ruto kutaka kuandaa mkutano wa chama ili kujadili na kutafutia ufumbuzi masuala tata ambayo yamezua mgawanyiko chamani.

Jana Dkt Ruto alisema kuwa serikali ya Jubilee imejitolea kuunganisha Wakenya na ndiposa walialika kiongozi wa ODM Raila Odinga serikalini ili kumwonyesha namna maendeleo yanavyofanywa badala ya kuandamana kila siku.

Dkt Ruto alikuwa amendamana na mwenyeji wake, mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro na wengine.

Lakini viongozi wa mrengo wa Kieleweke walipuuzilia mbali mwito wa kuacha siasa za migawanyiko wakisema ni Rais Kenyatta pekee anayeweza kuwaambia wanachopasa kufanya.