Ruto akubaliana na Raila kuwa kaulimbiu ya ‘hasla’ haifai kuharamishwa

Ruto akubaliana na Raila kuwa kaulimbiu ya ‘hasla’ haifai kuharamishwa

Na CHARLES WASONGA

KWA mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu Naibu Rais William Ruto ameonekana kukubaliana na hasidi wake wa kisiasa Raila Odinga kuhusu suala la sheria za siasa.

Dkt Ruto ameunga mkono kauli ya Bw Odinga kwamba mswada unaolenga kuharamisha kauli mbiu ya ‘hasla’ haufai.

Kupitia ujumbe katika akaunti yake ya Twitter, Dkt Ruto alisema anakubaliana na hatua ya Bw Odinga kutetea uhuru wa kujieleza unaolindwa na Katiba.

Hata hivyo, Naibu Rais ametofautiana na Bw Odinga kwamba matumizi ya kauli mbiu ya ‘mahasla’ yanaweza kusababisha migawanyiko ya kitabaka na fujo nchini.

“Nakubaliana na utetezi wake uhuru wa kujieleza unaolindwa na Katiba. Lakini kwa heshima hatukubaliana na fasiri yake potovu kuhusu dhima ya mahasla. Lakini tunaheshima mawazo yake. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa kauli mbiu ya hasla inaeleweza kwa uzuri,” akasema Dkt Ruto.

Naibu Rais alisema hayo saa chache baada ya Bw Odinga kuwaonya wabunge dhidi ya kupitisha mswada unaoharamisha matumizi ya kauli mbiu ya mahasla ambayo imekuwa ikutumiwa na Dkt Ruto na wandani wake katika mikutano yao ya kampeni.

Kamati ya Bunge kuhusu Usalama imedokeza kuwa itawasilisha mswada wa kuzima matumizi ya kaulimbiu hiyo inayohofiwa inaweza kuzua fujo baina ya Wakenya masikini na matajiri.

Hii inafasiriwa kama sehemu ya juhudi za kuzima kampeni hizo za Dkt Ruto zinazotaoa taaswira ya uwepo wa mgongano baina ya watu wa mapato ya chini na matajiri.

Mswada huo ukipitishwa na kuwa sheria kiongozi atakayepatikana na hatia ya kutumia kauli mbiu hiyo, atazuiwa kushikilia nyadhifa za umma. Adhabu zingine ni faini ya Sh5 milioni au kifunga cha miaka mitano gerezani.

Dkt Ruto na wandani wake hujichukulia kuwa mahasla huku wakiendeleza kampeni kwamba huu ni wakati ambapo watu wa tabaka hilo wanafaa kuwa na usemi katika ulingo wa uongozi.

Licha ya kwamba Bw Odinga ametetea uhuru wa Dkt Ruto na wenzake, kuendelea kutumia kauli mbiu hiyo, amewaonya Wakenya dhidi ya kuikumbatia.

“Matumizi ya kauli mbiu hii yanaweza kuleta fujo sawa na ilivyofanyika nchini Ujerumani wakati wa enzi ya kiongozi katili Adolf Hitler. Hitler alichochea mauaji ya halaiki kwa misingi ya matabaka ya kiuchumi, rangi na kabila,” akaonya.

“Wakenya wajiepushe nayo kwa sababu inaweza kusababisha machafuko nchini. Naamini kuwa wananchi watang’amua ukweli na kujitenga na udanganyifu huu,” akasema Bw Odinga.

You can share this post!

Raia waadhimisha miaka 10 ya kung’oa utawala wa Gaddafi

Wachuuzi wa ahadi hewa