Habari MsetoSiasa

Ruto akwepa kuandamana na Uhuru tena

July 7th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Naibu Rais William Ruto alikosa kuandamana na bosi wake, Rais Uhuru Kenyatta, alipotoa hotuba yake ya tisa kwa taifa kuhusu hali ya janga la Covid-19 Jumatatu.

Kama msaidizi mkuu wake mkuu, Dkt Ruto alitarajiwa kusimama kando ya Rais Kenyatta nje ya Jumba la Harambee akitoa masharti mapya ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona.

Hotuba hiyo ya ambayo Rais Kenyatta alitoa Jumatatu ilifuatiliwa kwa makini na Wakenya katika vyombo vya rasmi vya habari na mitandao mingine ya habari.

Lakini Naibu Rais hakuonekana popote. Badala yake Rais Kenyatta aliandamana na mawaziri Mutahi Kagwe (Afya), Profesa George Magoha (Elimu), Fred Matiang’i (Elimu) na wanachama wa baraza la viongozi wa kidini kuhusu Covid-19 wakiongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliko jimbo la Nyeri Antony Muheria.

Dkt Ruto alikosa kuandamana na Rais kwa shughuli hiyo muhimu wa kitaifa siku ambayo hasidi wake wa kisiasa katika Rift Valley Seneta Gideon Moi alikuwa nchini Malawi kumwakilisha Rais katika halfa ya kutawazwa kwa Rais mpya Lazarus Chakwera.

Mwanzoni mwa hotuba yake, Rais Kenyatta alisema aliongoza mkutano wa Baraza la Usalama (NSC) kwa ajili ya kuidhinisha maamuzi ambayo alitangaza kulegeza masharti ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Haikujulikana iwapo Dkt Ruto alihudhuria mkutano wa baraza hilo ikizingatiwa kuwa yeye ni mmoja wa wanachama wake.

Naibu Rais alionekana hadharani mara ya mwisho mnamo Jumamosi wiki jana alipowahutubia viongozi wa kidini na wanasiasa nyumbani kwake Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu.

Kwa mara ya kwanza, alalamikia kutishwa na kuhangaishwa kwa wandani wake.

Alikuwa akirejelea matukio ya hivi majuzi ambapo wabunge washirika wake walipokonywa nyadhifa za uongozi katika bunge la kitaifa na seneti. Vile vile, baadhi yao wamefikishwa mahakama kwa kashfa za ufisadi na wengine wanaendelea kuchunguzwa.