Habari Mseto

Ruto akwepa siasa na kuangazia corona

December 13th, 2020 1 min read

Na LUCY MKANYIKA

NAIBU Rais William Ruto alikwepa kuzungumzia siasa alipozuru Kaunti ya Taita Taveta, Jumapili na badala yake akiwahimiza Wakenya kujikinga na virusi vya corona.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kanisa la ACK St Peter’s Cathedral mjini Voi, Dkt Ruto alisema serikali inajikakamua kutatua masuala yanayokumba wahudumu wa afya ili kuzuia usambazaji wa ugonjwa huo.

“Ugonjwa huu unaweza kuzuiwa ikiwa kila mwananchi atafuata maagizo yaliyowekwa,” akasema.

Alisema serikali inaweka mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wako salama wanapofungua shule mwezi ujao.

Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit alisema kanisa litashirikiana na Wizara ya Elimu kusaidia katika ufunguzi wa shule mwaka ujao.

Askofu Sapit alisema watatoa ushauri na mwongozo kwa wanafunzi na walimu kuanzia Januari mwaka ujao. Askofu huyo alisema tayari wamefanya mazungumzo na wizara hiyo ili kutekekeza mpango huo katika shule zote kote nchini.