Ruto alenga ngome ya Raila kwa minofu

Ruto alenga ngome ya Raila kwa minofu

VICTOR RABALLA Na GEORGE ODIWUOR

RAIS William Ruto ameanza kumwaga minofu katika ngome ya mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 Raila Odinga, katika kinachoonekana kuwa juhudi za kuthibitishia nchi kwamba serikali yake haitabagua eneo lolote.

Kiongozi wa nchi Jumapili alizuru eneo la Nyanza kwa mara ya kwanza akiwa rais na kuahidi kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuimarisha maisha ya wakazi.

Eneo hilo lilimpigia kura Bw Odinga kwa wingi na haikutarajiwa Rais Ruto angelitembelea haraka na kuahidi kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Akihutubu baada ya kuhudhuria ibada katika kanisa la AIC mjini Homa Bay, Rais Ruto alisema serikali yake itabadilisha kaunti hiyo na eneo la Nyanza kwa jumula itakavyofanya katika maeneo mengine nchini.

“Serikali yangu itafanya kazi na kila mtu. Wale ambao hamkuniunga mkono. Ninawapenda wote,” Rais alisema.

Kama ishara kwamba serikali yake haitabagua sehemu yoyote, aliahidi kutembelea kaunti ya Homa Bay mwezi ujao kuzindua ujenzi wa nyumba 400 katika awamu ya kwanza inayolenga nyumba 5000 za bei nafuu.

“Nitarudi hapa mwezi ujao tuzindue awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu 400. Awamu zingine za ujenzi zitafuatia hadi tujenge nyumba 5000. Mradi huo utaunda nafasi za kazi kwa vijana,” alisema.

Rais Ruto ameahidi kwamba serikali yake itajenga nyumba 250,000 kote nchini na haikutarajiwa angeanza mradi huo katika ngome ya Bw Odinga.

Alifichua mpango wake wa kufufua miradi iliyokwama katika eneo hilo, ukiwemo ujenzi wa barabara muhimu ili kupiga jeki uchumi wa Homa Bay na Nyanza kwa jumula.

Baadhi ya miradi ya barabara ilianzishwa na serikali ya Jubilee aliyokuwa Naibu Rais.

Alisema kwamba kuna kilomita 200 za barabara zilizokwama na akaahidi kutenga pesa katika bajeti ili kukamilisha ujenzi wake.

Miongoni mwa barabara hizo ni ya kutoka Kanyadhiang-Pala- Kadel aliyeanzisha 2018 lakini ujenzi ukakwama.

Nyingine ambayo aliahidi itawekwa lami ni ya Mbita- Sindo-Magunga-Sori inayounganisha vijiji vya kaunti za Homa Bay na Migori.

“Ninajua baadhi ya miradi ya barabara katika kaunti hii imekwama. Ninawaomba mnipe muda nipange bajeti na uchumi na kisha nije hapa tukamilishe miradi hiyo,” alisema Rais.

Rais alisema kwamba serikali yake itasaidiana na viongozi wa eneo hilo kuimarisha miradi ya maji na usafi katika miji ya Homa Bay Kendu Bay, Sindo, Rangwe na Karachuonyo.

Aidha, kiongozi wa nchi alisema kwamba serikali yake itaanzisha miradi ya kuongeza thamani bidha za kilimo katika Nyanza, kuwapa wakulima mbegu za pamba zinazotoa mavuno mazuri na kuimarisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.

“Nimeita mkutano wa baraza la mawaziri Jumatatu kuidhinisha mbegu bora ambazo wanasayansi wetu wamepitisha ambazo zinastahimili magonjwa na wadudu. Tunataka wakulima wetu wa pamba wanufaike ili kukuza sekta ya viwanda. Hii ni serikali yenu, nitafanya kazi na kila mtu,” alisema.

Akisema kwamba vijana wanahitaji kusaidiwa kuwa na ujuzi ili waweze kupata nafasi za kazi, Rais Ruto alisema kwamba chuo cha kiufundi kitajengwa eneo hilo.

“Eneo bunge la Homa Bay Town halina chuo cha kiufundi, hata Suba Kusini. Nitazungumza na viongozi watenge ardhi ya ujenzi wa vyuo ili vijana waweze kunufaika,” alisema.

Rais Ruto alihimiza viongozi waliochaguliwa kusahau malumbano ya wakati wa kampeni na kuungana kufanya kazi ili kunufaisha Wakenya wanaotaka maendeleo.

Alikuwa ameandamana na mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, mwenzake wa Ugenya David Ochieng, Marwa Kitayama (Kuria Mashariki) na Mathias Rhobi (Kuria Magharibi), waliokuwa magavana Jack Ranguma (Kisumu), Okoth Obado (Migori) na waziri mteule wa Habari na Mawasiliano Bw Eliud Owalo.

Ziara hiyo hata hivyo haikuhudhuriwa na viongozi wengi wa siasa kutoka Homa Bay.

Gavana Gladys Wanga alisema hangeweza kuhudhuria hafla hiyo kwani yuko jijini Mombasa shughuli rasmi za kikazi.

“Ninamkaribisha rais kwa niaba ya wakazi wa Homa Bay. Ninamwomba ajihisi nyumbani,” akasema Bi Wanga.

Mbunge wa Suba Kaskazini Millie Odhiambo, mwenzake wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma na Seneta Moses Kajwang walisema hawakuwa wamealikwa katika hafla hiyo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Visasi na chuki ni vikwazo kwa nchi kuendelea

JIJUE DADA: ‘Kuchomeka’ wakati wa kukojoa...

T L