Ruto alia ‘mahasla’ wanamfyonza

Ruto alia ‘mahasla’ wanamfyonza

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto sasa analalamika kuwa wapigakura wanatumia ukarimu wake kujinufaisha wanapotaka maendeleo, kisha kumhepa wakati wa uchaguzi.

Dkt Ruto amekuwa akifanya harambee nyingi kote nchini akidai anatumikia Mungu na vile vile, amejitolea kusaidia walalahoi kupanda daraja kimaisha.

Hata hivyo, sasa imebainika wazi kuwa ukarimu wake huo hauhusu kujitafutia makao mbinguni anapojenga makanisa, wala kutaka kupokea baraka kwa mkono mmoja wakati mwingine unapotoa kwa maskini.

Akizungumza akiwa Kaunti ya Busia mwishoni mwa juma, Dkt Ruto alilaumu wakazi wa eneo la Magharibi mwa Kenya kwa kumtumia vibaya.

Alisema wanamtafuta wanapotaka maendeleo na kukataa kumuunga mkono wakati wa uchaguzi unafika, ishara kuwa anapotoa huwa anatarajia atazoa umaarufu wa kisiasa hasa anapomezea mate urais mwaka ujao.

Dkt Ruto alisema wakazi wa eneo hilo ni wepesi wa kumtafuta wanapotaka asaidie katika miradi mbalimbali ya maendeleo lakini wakati wa uchaguzi, wanamuacha na kumpigia kura kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

“Nyinyi mnanitumia vibaya. Kwa sababu sasa ikifika siku ya maendeleo, mkitaka kanisa lijengwe, mkitaka barabara, mkitaka basi la shule mnatafuta Ruto. Lakini ikifika siku ya kupiga kura, mnaanza maneno ingine ya kitendawili, sijui oh tibim, sasa, hapana, hapana,” Dkt Ruto alisema alipozuru Funyula Kaunti ya Busia.

Tibim ni msemo unaohusishwa na chama cha ODM chake Bw Odinga wakati wa kampeni za uchaguzi.

Dkt Ruto amekuwa akiongoza hafla za kuchangia makanisa na makundi ya vijana na wanawake katika mbinu ya kuvumisha azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Wapinzani wake wanapomtaka aeleze anakotoa mamilioni anayotumia kuchanga kwa harambee, huwa anawaambia anafanya kazi ya Mungu kwa sababu amemtoa mbali.

“Baadhi yetu tunasababu ya kumshukuru Mungu na kufanya kazi yake kwa kuwa tunajua alikotutoa,” Dkt alimjibu Bw Odinga wakati mmoja.

Baadhi ya wabunge wa eneo la Magharibi ni wanachama wa vuguvugu lake alilobuni kujipigia debe akidai anajali maslahi ya Wakenya masikini.

Tangu 2018, Dkt Ruto amekuwa akitumia harambee kupenya ngome za Bw Odinga anayemchukulia kuwa mpinzani wake mkuu kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, mwaka jana, alisitisha hafla za harambee kufuatia kuongozeka kwa maambukizi ya virusi vya Corona.

Tangu uchaguzi mkuu wa 2007, eneo la Magharibi limekuwa likimpigia Bw Odinga kura kwa wingi. Dkt Ruto alisema licha ya ukarimu wake, wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakimuunga Bw Odinga.

Aliwataka walipe ukarimu wake kwa kumuunga mkono kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Alitetea juhudi zake za kusaidia masikini kujiinua kiuchumi na kuwataka wakazi wapuuza wapinzani wake

“Nilimsikia jamaa mwingine juzi akisema hawa mahsla, watu wa pikipiki eti ni takataka. Mimi nataka nimwambie huyo muungwana, wewe wachana na bodaboda, wachana na watu wa mkokoteni na wilibaro. Hiyo ni biashara pia kama ile nyingine,” alisema.

Bw Odinga amekuwa akimlaumu Dkt Ruto kwa kudunisha Wakenya kwa kuwapatia wilbaro na pikipiki badala ya kuunga mageuzi ya katiba anayodai yatahakikishia vijana maisha bora.

Akizungumza katika mikutano ya kupigia debe mchakato huo wa marekebisho ya katiba katika mitaa ya Burma, Kayole na Githurai, Bw Odinga alitaja vuguvugu la hasla kama takataka.

You can share this post!

Corona imeathiri uwezo wa wanaume kuzalisha – Utafiti

Adhabu ya kiboko shuleni yapingwa