Habari za Kitaifa

Ruto alia presha za Gen Z zilisababisha aingize ODM serikalini


RAIS William Ruto amesema serikali aliyoiunda hivi maajuzi ya kuwateua maziri wapya, wakiwemo wanne kutoka chama cha ODM si serikali ya muungano wa vyama bali unalenga umoja wa Wakenya.

Kiongozi wa taifa, Jumatatu, Agosti 12, 2024 kwenye ziara yake katika eneo la Gusii, alisema ilifikia wakati ambapo maslahi ya taifa hili yangewekwa mbele kuliko kiongozi yeyote au chama.

“Inafika mahali, ambapo cha muhimu si maslahi ya kiongozi au chama bali kuleta umoja na manufaa kwa Wakenya. Ndio maana mliona tukiunda serikali mpya,” Rais Ruto alisema katika eneo la Kiabonyoru, eneobunge la Mugirango Kaskazini, Kaunti ya Nyamira.

Dkt Ruto alitumia muda wake mwingi kwenye ziara hiyo kuwaelezea Wakenya kuhusu maamuzi aliyochukua kwa kuwajumuisha viongozi wa upinzani katika baraza lake la mawaziri na akawaomba wamuunge mkono.

Haya yalichangiwa na maandamano ya vijana wa Gen Z, yaliyodumu zaidi ya miezi miwili kulalamikia utawala wa wake.

“Hatutaki tena siasa za migawanyiko. Cha muhimu sasa ni kuwahudumia Wakenya kwa kuwaunganisha na kulisukuma taifa letu mbele,” Dkt Ruto alisema.

Kiongozi wa taifa aliandamana na naibu wake Rigathi Gachagua, Waziri wa Elimu Migos Ogamba, magavana Simba Arati (Kisii), Amos Nyaribo (Nyamira) na wabunge wengine kutoka eneo pana la Gusii.

Katika sehemu za Kenyerere, eneobunge la Kitutu Masaba, Dkt Ruto alizitaka asasi zote za serikali kufanya kazi kwa ukaribu bila malumbano.

Kauli ya Rais Ruto kuhusu serikali jumuishi anayotetea inaleta taswira ya umoja wa Kenya, inajiri wakati ambapo wandani wa Bw Gachagua wanakosoa wanasiasa wa ODM kushirikishwa kwenye serikali ya Kenya Kwanza.

Wandani sita wa kinara wa chama hicho, Bw Raila Odinga waliteuliwa katika Baraza la Mawaziri ambalo lilitangazwa na Rais Ruto Julai 2024, ili kutuliza maandamano ya Gen Z.