HabariSiasa

Ruto alinisaidia Uhuru aliponiacha kwa baridi – Nyoro

December 15th, 2019 2 min read

NA NDUNGU GACHANE

MBUNGE wa Kiharu Ndindi Nyoro amesema kwamba aliondoka kwenye kambi ya Rais Uhuru Kenyatta baada ya kushindwa kumfikia mara kadhaa alipohitaji msaada wake.

Kwenye mahojiano ya kipekee, alikariri kwamba hatayumbishwa kamwe kuendelea kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto kwani ndiye alimsaidia hata wakati walikuwa hawajuani vyema.

Alisema anaweza tu kukoma kumfuata Dkt Ruto kama naibu rais ataamua kujiunga na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye kulingana naye, hawezi kuaminika.

Mwanasiasa huyo ameapa kwamba ataendelea kumvumisha Naibu Rais kama anayefaa kutwaa wadhifa wa kiongozi wa nchi 2022 kwa kuwa ni kiongozi ambaye anaweza kufikiwa kwa urahisi akilinganishwa na Rais Kenyatta.

Bw Nyoro anayehudumu muhula wake wa kwanza bungeni, alisema kwamba ataendelea kusalia wima nyuma ya Dkt Ruto hata baada ya kuandamwa na vitengo vya Tume ya Maadili ya Kupambana na Ufisadi (EACC) na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) siku za nyuma.

Aidha alisimulia kwamba ukuruba wake na Naibu Rais ulianza pale alipokuwa akitafuta kuchaguliwa mwenyekiti au naibu mwenyekiti wa kamati fulani ya bunge ambapo alishindwa kumfikia Rais lakini akamfikia Dkt Ruto kwa urahisi mno.

Mbunge huyo wa mrengo wa Tangatanaga anasema licha ya jitihada zake zote za kujaribu kumfikia Rais mara kadhaa, alifeli pakubwa kwa kuwa iliaminika kiongozi wa nchi angeweza kupokea ujumbe kupitia tu aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na Bw Njee Muturi.

“Nilikuwa nawapigia simu mara kadhaa na kuwatumia arafa lakini sikuwa nimewaeleza kile nilichohitaji japo niliwaambia nilihitaji msaada wao kuhusu suala fulani. Hata hivyo, hawakupokea simu au kujibu arafa zangu kwa wiki kadhaa. Niliona walikuwa na shughuli nyingi na hawakuwa na nafasi ya kunijibu ndiposa nikakata tamaa kwamba hata Rais mwenyewe hafikiki,” akasema Bw Nyoro.

“Wakati huo sikumjua Dkt Ruto binafsi kwa kuwa hatukuwa tumekutana ndipo nikamtumia ujumbe kwa kujieleza na akanipigia simu baada ya muda mfupi. Ingawa sikupata kile nilichohitaji, alinivutia kutokana na jinsi alivyozungumza nami na kunishughulikia. Hivyo ndivyo viongozi wanafaa kuwa ili kuimarisha uhusiano wao na raia,” akaongeza Bw Nyoro.

Kiongozi huyo alifichua kwamba umri wake bado ni mdogo na njia ya pekee ya kukwea ngazi ya umaarufu wa kisiasa ni kujinasibisha na Naibu Rais ambaye alimtaja kama ‘mwalimu wake wa kisiasa’.

“Nahitaji mwongoza na siwezi kusoma kitabu kuhusu Uhuru ili nijifunze mengi kuhusu siasa. Nahitaji mfano halisi na mtu wa kuniongoza si mwengine ila Dkt Ruto,” akasisitiza.

Alifunguka na kusema amepokea malezi ya kisiasa mikononi mwa watangulizi wake waliowakilisha eneo bunge hilo, akiwataja marehemu Kenneth Matiba, Ngenye Kariuki na Seneta Irungu Kangata kama waliomkuza hadi akawa mbunge.