‘Ruto alishika Uhuru mateka’

‘Ruto alishika Uhuru mateka’

Na JUSTUS OCHIENG

KINARA wa ODM, Raila Odinga, amesimulia jinsi alivyomnusuru Rais Uhuru Kenyatta kutoka “mateka” aliyowekwa na Naibu wake William Ruto katika muhula wa kwanza wa utawala wa Jubilee, akisema mwafaka kati yake na Rais uliokoa nchi.

Bw Odinga alisema serikali ya Jubilee ilizongwa na ufisadi katika muhula wa kwanza wa utawala wake huku mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2017 ukifanya hali kuwa mbaya zaidi.

Hii ni kutokana na ghasia zilizosababisha maafa na uharibifu mkubwa wa mali nchini.

Hata hivyo, Dkt Ruto alimjibu kwa kupuuzilia mbali madai hayo akishikilia kuwa, ni Bw Odinga na vinara wenzake wa uliokuwa muungano wa NASA waliovuruga mipango ya maendeleo serikalini.

“Ni wakati huu ambapo Uhuru anajaribu kutekeleza ajenda yake ya maendeleo kwa sababu amepata utulivu. Nilipata akiwa amekamatwa koo. Nyoka imetoka. Sasa anaweza kupumua na kuelekeza juhudi zake katika masuala ya maendeleo,” Bw Odinga alisema katika makao makuu ya chama chake, Chungwa House, Nairobi, alipopokea wanasiasa waliohama vyama vyao na kujiunga na ODM.

Huku akirejelea hatua ya Dkt Ruto na wandani wake kuhama Jubilee na kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA), waziri huyo mkuu wa zamani alisema Wakenya sasa wanaweza kushuhudia utekelezaji wa miradi kadha ya maendeleo.

“Walisema sisi ni ‘analogu’ na kwamba, wao ni dijitali na hata wakaahidi kuwa watawapa wanafunzi wote wa darasa la kwanza, tarakilishi. Waliahidi kujenga viwanja vya michezo katika kaunti zote, je, mumeviona? Ni sasa ambapo Uhuru anajaribu kutekeleza ajenda zake,” Bw Odinga akaeleza.

Alisema huu ndio wakati Rais Kenyatta anatumia muda mfupi uliosalia kukamilisha miradi kadha ya ujenzi wa barabara, nyumba za gharama ya chini na viwanja vya michezo walivyoahidi katika muhula wa kwanza.

“Utekelezaji wa miradi unaoendelea kutekelezwa sasa haukuwepo katika muhula wa kwanza wa utawala wa Jubilee kutokana na kukithiri kwa sakata za ufisadi,” akasema.

Lakini Dkt Ruto akihutubia ujumbe wa viongozi wa mashinani kutoka jamii ya Abagusii, wanaoishi Nairobi, naibu huyo wa rais alimjibu Bw Odinga akisema ni yeye (Raila na wenzake wa Nasa waliovuruga serikali ya Jubilee.

“Ningetaka kuuliza marafiki zetu waliokuwa Nasa. Wanajaribu kutafuta makosa kutoka kwetu. Wanafaa kuwa na heshima kwa sababu tulifanya kampeni na tukaunda serikali hii lakini waliingia na kuanza kuendeleza masilahi yao ya kibinafsi. Mbona uikosoe serikali ilhali ulivuruga mipango yetu ya Ajenda Nne Kuu na mkaanzisha vipaumbele tofauti vya ugavi wa mamlaka na vyeo? Mambo hayo hayakuwa sehemu ya mpango wetu baada ya ushindi wetu 2017,” Dkt Ruto akasema.

Baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kusitisha uhasama wao kupitia handisheki mnamo Machi 9, 2018, vinara wengine wa Nasa kama vile Kalonzo Musyoka (Wiper), Musalia Mudavadi (ANC) na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula pia walikubali kushirikiana na serikali.

Ni kiongozi wa Chama cha Mashinani (CCM) Isaac Ruto pekee aliyetangaza kuunga mkono misimamo ya kisiasa ya Dkt Ruto.

“Ni vinara wa Nasa wakiongozwa na Raila waliovuruga mipango yetu ya Agenda Nne. Mlitupeleka katika reggae na BBI kubadilisha katiba ili mpate nafasi zaidi za uongozi kwa sababu mlikuwa wengi,” Naibu Rais akaongeza.

You can share this post!

Polo auguza nyeti kisiri nyumbani

MATHEKA: Viongozi wasitumie ukame kujikweza kisiasa raia...