Ruto alivyokwepa ulaghai wa kisiasa

Ruto alivyokwepa ulaghai wa kisiasa

RAIS William Ruto alifanya mashauriano ya kina na wazi, na washirika wake kabla ya kuzindua Baraza la Mawaziri mnamo Jumanne, hatua ambayo iliepusha malalamishi kutoka kwa waliokosa kupendekezwa kwa nyadhifa hizo.

Kulingana na wandani wake, mashauriano hayo yalianza hata kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9 na kuendelea baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo.

Kilichoibuka katika orodha ya majina aliyopendekeza ni kuwa, Rais Ruto ni kiongozi wa kutimiza ahadi kwa washirika wake wanaodhihirisha uaminifu wa dhati kwake.

Alipokuwa akiunda miungano na vigogo wa vyama tofauti kabla ya uchaguzi, Dkt Ruto alikuwa akisema ‘hatawaruka’ kamwe wakimsaidia kuingia mamlakani.

“Enzi za ulaghai wa kisiasa zimeisha. Kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu, tutaunda serikali pamoja,” alisema mara si moja katika kampeni zake hasa katika ngome za washirika wake Mlima Kenya na Magharibi mwa Kenya.

Ili kuzuia uasi, alihakikisha kila sehemu iliwakilishwa katika Baraza la Mawaziri.

Katika eneo la Pwani alipendekeza watu wawili kuwa mawaziri, wawili katika eneo la Ukambani, saba eneo la Mlima Kenya, watano eneo la Rift Valley, mmoja kutoka kaskazini Mashariki, watatu kutoka Magharibi na wawili kutoka Nyanza.

Alipokuwa akitaja majina ya watu alioteua wawe mawaziri, Rais Ruto alisema ushindi wa muungano wake wa Kenya Kwanza ulikuwa ushindi wa Kenya nzima huku akitambua wanasiasa waliomuunga mkono tangu alipotangaza azma yake ya urais na kuhangaishwa na serikali ya chama cha Jubilee.

Ili kuepusha malalamishi na mgawanyiko unaotokana na kuhisi kusalitiwa, Dkt Ruto alizungumza na wandani wake kabla ya kufanya uteuzi.

Kulingana na Mwakilishi wa Kike wa Uasin Gishu, Gladys Shollei, ingawa Rais Ruto alishauriana na washirika wake kwa mapana, alifanya uamuzi wa mwisho kuhusu aliyetaka kuwa katika Baraza lake la Mawaziri.

TAHADHARI

Akizungumza katika kipindi kimoja cha runinga Ijumaa asubuhi, Bi Shollei alisema japo baadhi ya waliopendekezwa kuwa mawaziri walichaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita, ilikuwa ni kuchukua tahadhari.

“Mtu hangeweza kuambiwa asigombee kwa sababu alikuwa amehakikishiwa nafasi hiyo. Yalikuwa mazungumzo hadi dakika ya mwisho na hakuna mtu angeweza kuzuiwa kugombea,” alisema.

Mbunge huyo alisema kugombea kwao kulikuwa mkakati wa kisiasa ili wasikose kura za maeneo yao.

Baadhi ya wabunge walioteuliwa katika baraza la mawaziri ni pamoja na Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome (Maji), seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen (Barabara), Mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale (Ulinzi) na Seneta Maalum, Bi Soipan Tuya (Mazingira).

Rais Ruto aliheshimu makubaliano yake na viongozi wa vyama tanzu vya muungano wa Kenya Kwanza kwa kuhakikisha Moses Wetang’ula amechaguliwa spika hata baada ya kushinda useneta wa Bungoma.

Aidha, alipendekeza kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi kuwa Mkuu wa Mawaziri, mwenzake wa Maendeleo Chap Chap, Dkt Alfred Mutua kuwa waziri wa Mashauri ya Kigeni. Mshirika wake mwingine, Moses Kuria wa Chama Cha Kazi, alipendekezwa kuwa waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda.

Na imeibuka kuwa anarai viongozi wa vyama tanzu waliopendekezwa kuwa mawaziri kuvunja vyama vyao na kujiunga na chake cha UDA.

Hii itatia nguvu chama chake, kuimarisha uaminifu na kuondoa uasi unaoweza kuzuka. (Soma habari tofauti)

Katibu Mkuu wa UDA, Veronica Maina alisema wanaovunja vyama vyao wanafanya hivyo kwa hiari. Hii inamaanisha iwapo vyama tanzu vitavunjwa, muungano wa Kenya Kwanza utaisha na UDA kubaki chama tawala pekee.

Taifa Jumapili imebaini Dkt Ruto anafanya hivi kupitia mashauriano.

“Rais Ruto alitumia mashauriano kuepusha malalamishi ambayo yamekumba na kusambaratisha miungano mingi ya kisiasa baadhi ya washirika wakihisi kusalitiwa. Hii ndiyo siri inayofanya Kenya Kwanza kuwa tofauti na miungano mingine iliyotawala Kenya na hata ile ambayo haikuingia mamlakani,” alisema mbunge mmoja wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambaye aliomba tusitaje jina akisema haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya rais au chama.

Alisema lengo la Rais Ruto ni kudumisha umoja na uthabiti wa muungano wake wa Kenya Kwanza na kuwa na serikali inayoakisi sura ya kitaifa.

“Hii itajitokeza katika uteuzi wa nyadhifa nyingine kama makatibu wa wizara, wakuu wa idara na mabalozi. Itakuwa serikali ya Wakenya wote kinyume na wanavyotarajia wapinzani, alivyosema rais kwa kuwa hataki ulaghai wa kisiasa,” akasema mbunge huyo.

You can share this post!

Montreal anayochezea Wanyama yazidi kutesa wapinzani MLS

Njama ya UDA kumeza vyama tanzu katika Kenya Kwanza...

T L