Habari Mseto

Ruto aliwahi kuniahidi kuniteua kama mgombea-mwenza 2022, adai Waititu

February 7th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, amedai kwamba Rais William Ruto aliahidi kumteua kama mgombea-mwenza wake kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Bw Waititu alidai alipewa ahadi hiyo na Rais Ruto pamoja na magavana wa zamani Kiraitu Murungi (Meru) na Francis Kimemia (Nyandarua).

Kwenye mahojiano Jumatatu jioni, Bw Waititu alisema walipewa ahadi hiyo na Rais Ruto kwenye mkutano wa faragha aliowaita watatu hao, akiwarai kumuunga mkono kuwania urais dhidi ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, aliyekuwa akiungwa mkono na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Rais Ruto alituita kwenye mkutano wa faragha wakati kampeni za mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja zilikuwa zimechacha. Aliturai kumuunga mkono, akiahidi kwamba angemteua mmoja wetu kuwa mgombea-mwenza wake,” akasema Bw Waititu, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni.

Bw Waititu alisema hajui ni vipi Rais Ruto alibadilisha uamuzi wake, kwa kumteua Bw Rigathi Gachagua kama mgombea-mwenza wake.

“Tulingoja sana Ruto atimize ahadi yake. Pengine mielekeo na mazingira ya kisiasa yalibadilika, kwani wenzangu walivuka katika kambi ya Azimio, na kumuunga mkono Bw Odinga,” akasema kiongozi huyo.

Bw Waititu alipoteza kiti chake cha ugavana 2020 baada ya madiwani kupiga kura ya kutokuwa na imani naye na baadaye Seneti ikapiga kura kuunga mkono hatua hiyo.

Bw Murungi aliunga mkono Azimio kupitia chama chake cha Devolution Empowerment Party (DEP).

Bw Kimemia, kwa upande, wake pia alimuunga mkono Bw Odinga. Alitetea nafasi ya ugavana Nyandarua, lakini akashindwa na Gavana Kiarie Badilisha wa chama tawala cha UDA.

Bw Waititu pia aliilaumu serikali, akidai ilimdanganya kwamba ingemsaidia kukabiliana na kesi za ufisadi ambazo zimekuwa zikimkabili.