Habari Mseto

Ruto amhepa Uhuru tena

November 26th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto jana Jumatano alikosa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji wa sahihi za mageuzi ya katiba kupitia mchakato wa BBI katika jumba la KICC, Nairobi.

Hii ilikuwa mara yake ya pili mwaka 2020 kutohudhuria hafla iliyoongozwa na Rais licha ya waandalizi kusema alialikwa.

Mapema mwaka 2020, hakuhudhuria kongamano kuhusu janga la corona, kiti chake kikabaki wazi ukumbini.

Kiranja wa Wachache bungeni, Bw Junet Mohammed aliambaia Taifa Leo kwamba Dkt Ruto alialikwa lakini “hakuthibitisha kuwa angefika.”

“Ni baada ya hapo ambapo makarani wetu waliondoa jina lake kwenye ratiba rasmi ya wanenaji,” akasema Bw Mohammed aliye mwenyekiti-mwenza wa kamati simamizi ya mchakato wa BBI.

Kiti kimoja kilichoonekana wazi baina ya Rais Kenyatta na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ilidaiwa kuwa ndicho alichotengewa Dkt Ruto.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Spika wa Seneti Kenneth Lusaka, mawaziri, magavana na wabunge wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Pia walikuwapo viongozi wa vyama vingine vya kisiasa kama vile Musalia Mudavadi (ANC), Moses Weteng’ula (Ford Kenya), Gideon Moi (Kanu), Dkt Alfred Mutua (Maendeleo Chap Chap) na kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyeripotiwa kusafiri ng’ambo, aliwakilishwa na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Farah Maalim.

Dkt Ruto ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa mapendekezo yaliyomo kwenye BBI alihudhuria hafla ya uzinduzi wa ripoti ya pili ya BBI Bomas mnamo Oktoba 20,2020.

Alitumia fursa hiyo kudondoa mapungufu kadha katika ripoti hiyo.