Habari

Ruto amkaidi askofu kanisani

September 21st, 2020 2 min read

LEONARD ONYANGO na VALENTINE OBARA

NAIBU wa Rais William Ruto alitumia ujanja Jumapili kukaidi agizo la Askofu wa Kanisa la Africa Inland (AIC), jijini Nairobi aliyekuwa ameagiza viongozi wasizungumzie masuala ya siasa kanisani.

Kiongozi wa Kanisa la AIC, Askofu Abraham Mulwa alikuwa ameonya wanasiasa waliohudhuria hafla ya ibada ya kumtawaza Askofu Joshua Kimuyu kuwa kiongozi wa AIC Kaunti ya Nairobi, kwamba kanisa hilo huwa haliruhusu wageni na waumini kuzungumzia siasa wanapohutubu ndani ya kanisa.

“Usitoe kauli zozote za kisiasa. Hapa mbele ni mapasta tu wanaruhusiwa kusimama lakini nimekupa heshima tu useme machache kwa dakika tatu,” Askofu Mulwa akaonya, wakati aliyekuwa mbunge wa Kilome Regina Ndambuki alizungumza.

Askofu alirudia onyo sawa na hilo wakati mbunge wa Embakasi Kaskazini, James Gakuya alipotakiwa kutambulisha wabunge zaidi ya 15 wa kundi la Tangatanga walioandamana na Dkt Ruto.

“Mheshimiwa, uwanja ni wako lakini kumbuka hili ni kanisa la AIC na hakuna siasa,” akasema Askofu Mulwa.

Viongozi wachache ndio waliruhusiwa kuzungumza akiwemo Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana ambaye alimwalika Dkt Ruto.

Wakati Naibu Rais aliposimama kuhutubu, aliungama kwamba anafahamu vyema Kanisa la AIC huwa haliruhusu siasa ndani ya kanisa.

“Mimi nikiwa muumini wa Kanisa la AIC, tulifundishwa kuwa siasa haizungumzwi kanisani. Mimi naelewa hilo sana,” akasema.

Alianza kwa kuongoza wimbo, kisha akakariri vifungu katika Biblia lakini ‘mahubiri’ yake yalionekana kulenga siasa za nchi.

Katika mahubiri yake, Dkt Ruto alirejelea jinsi katika Biblia watu ambao hawakuthaminiwa, wakapitia mateso, ndio baadaye walibobea wakawa wafalme.

Machoni mwa wadadisi, fumbo hili ambalo yeye hurejelea mara nyingi akikutana na viongozi wa kanisa hulenga kuashiria safari yake kuelekea Ikuluni ifikapo 2022.

Dkt Ruto vile vile, alizungumzia suala la ushindani kati ya walala hoi (hustler) na mabwanyenye ambao unaendelea kukashifiwa na viongozi wanaomlaumu kutumia umaskini kujikuza kisiasa.

“Hata mtoto wa maskini anaweza kuibuka akawa mtu wa maana hii Kenya,” akasema.

Kwa muda mrefu sasa, Naibu Rais amekuwa akikutana na makundi ya vijana na kina mama nyumbani kwake Karen, Nairobi ambapo huwapa misaada ya kujikuza kibiashara.

Ingawa yeye husema misaada hiyo ni ya kuwainua kimaisha, mahasimu wake husema ni kusudi la kujipendekeza anapojiandaa kujaribu bahati yake kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ifikapo 2022.

Kando na hayo, hakukamilisha hotuba yake kabla kutumia ujanja tena kukosoa Mpango wa Maridhiano (BBI) unaopigiwa debe na Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Huku akiepuka kuwataja viongozi hao wawili wala BBI moja kwa moja, Dkt Ruto alisema kwa sasa nchi inafaa kujali kutatua changamoto zinazokumba raia badala ya kutaka marekebisho ya katiba.

“Wale wengine wamekubaliana nasi kwamba idadi kubwa ya Wakenya wanahangaika. Tunachohitaji wakati huu ni mipango itakayowezesha Wakenya kupata ajira, makazi bora na kuinua biashara zao. Mambo ya vyeo na mamlaka yatakuja baadaye,” akasema Dkt Ruto.

Kauli yake ilionekana kumlenga Bw Odinga, ambaye kwa siku kadha sasa amekuwa akisisitiza kuwa Wakenya wote ni walala hoi kwani hata mabwanyenye walianzia chini kimaisha, kwa hivyo haifai Dkt Ruto kuwagawanya vikundi viwili.

Alitumia ujanja huo huo wa mafumbo na misemo kukashifu jinsi watu hufurushwa kiholela kutoka maeneo mbalimbali ya Nairobi ikiwemo makazi na sehemu za biashara, akitaka walala hoi kuheshimiwa.

Wakati huo huo, alionekana kukashifu jinsi wandani wake wamekuwa wakikamatwa na polisi huku wengine wao wakidai kutishiwa kufunguliwa mashtaka kwa sababu wanampigia debe.

“Kwa kuwa tumekubaliana kwamba nchi hii ni ya watu maskini, tuepuke matusi, vitisho na tuheshimu kila mlala hoi. Tujue kwamba sote tuko sawa. Wauzaji mitumba, wahudumu wa bodaboda na vinyozi wote ni wamoja,” akasema Dkt Ruto. Gavana Kibwana alimtaka Naibu wa Rais Ruto kufanya mazungumzo na Rais Kenyatta na Bw Odinga ili kuhakikisha kuna amani nchini hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022.