Ruto amlima Uhuru

Ruto amlima Uhuru

WANDERI KAMAU na LEONARD ONYANGO

NAIBU wa Rais William Ruto alitumia ziara yake katika eneo la Kisii kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta – hatua inayodhihirisha kwamba urafiki baina ya viongozi hao wawili hauwezi kufufuliwa tena licha ya wito wa maaskofu kutaka kuwapatanisha.

Akihutubu wikendi kwenye kikao cha faragha na viongozi wanaomuunga mkono katika Kaunti ya Kisii, Dkt Ruto alisema kwamba serikali ya Rais Kenyatta ilipoteza dira ya maendeleo tangu 2018 alipotangaza kushirikiana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia kwa handisheki.

Alimkosoa Rais Kenyatta na Bw Odinga kwa akisema kwamba handisheki haikuleta amani nchini. Badala yake, Dkt Ruto alidai, ilivuruga amani ndani ya chama cha Jubilee.

“Kuna wageni (Bw Odinga na viongozi wengine wa uliokuwa muungano wa NASA) waliotutembelea. Walikuja na mapepo kwani walivuruga kila ajenda tuliyokuwa nayo kubadilisha maisha ya Wakenya. Walikuja na mapepo ambayo yalisababisha wakuu wa chama kutimua wanachama wake huku wabunge wakipokonywa nyadhifa Bungeni. Je, hiyo ndiyo amani iliyoletwa na wageni?” akauliza.

Kwenye kikao hicho, Dkt Ruto alisema moja ya mipango iliyovurugika ni ule wa ujenzi wa nyumba 500,000 walizolenga kumaliza kufikia mwaka 2022 ili kuwasaidia Wakenya kupata makazi bora kwa bei nafuu.

Alisema kwamba kufikia sasa, serikali imefaulu kujenga nyumba 3,000 pekee.

Aidha, aliongeza kwamba serikali imefeli kutimiza ahadi yake ya kuboresha sekta nyingine muhimu kama vile afya na kilimo.

“Ikiwa huu ungekuwa mtihani, ni wazi serikali imefeli kabisa. Tatizo kuu ni kwamba tuliacha masuala muhimu na kuegemea shughuli za Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI),” akaeleza.

Alisema kuwa kutokana na mvurugiko uliotokana na handisheki, Chama cha Jubilee (JP) kilisambaratika kabisa na kuanza kuwahangaisha wanachama wake.

Aliongeza kwamba baada ya uchaguzi wa 2017, chama kilikuwa na karibu wabunge 170, lakini sasa kimebaki na wabunge kati ya 20 na 25.

“Tulipoanzisha Jubilee, tulikuwa na lengo la kukifanya kuwa chama cha kitaifa, kinyume na hali ambayo imekuwepo ambapo vyama vingi hubuniwa kwa misingi ya kikabila. Ni kwa ahadi hiyo ambapo Wakenya walituunga mkono kikamilifu na kuwachagua wabunge wengi zaidi ikilinganishwa na vyama vingine. Hata hivyo, chama kiligeuka kuwa jukwaa la vitisho na usaliti. Matunda ya handisheki yalikuwa ni kufukuzwa kwa viongozi chamani na wengine kutolewa katika kamati za Bunge na Seneti,” akasema Ruto.

Alipuuzilia mbali juhudi zinazoendeshwa kuunganisha Jubilee na ODM, akikitaja chama cha Jubilee kama kisicho na ushawishi wowote.

Licha ya mpango wa BBI kuanzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga, Dkt Ruto aliutaja kuwa “ulaghai mkubwa zaidi wa kisiasa kuwahi kushuhudiwa nchini.”

Kauli hiyo ni licha ya Rais Kenyatta kusisitiza kwamba mpango huo ulilenga kuwafaidi Wakenya kwa kuongeza mgao wa fedha unaotumwa katika serikali za kaunti.

“BBI ilikuwa njama ya kuturudisha katika enzi ya Rais mwenye mamlaka kupindukia. Hii ni licha ya Wakenya kupinga hilo kupitia harakati za kushinikiza mageuzi ya kikatiba kwa zaidi ya miaka 30,” akasema.

Hapo Jumapili, Dkt Ruto pia alijitetea vikali dhidi ya lawama za kukataa kushiriki mazungumzo ya kutafuta muafaka kati yake na Rais Kenyatta yaliyoitishwa na maaskofu wa kanisa Katoliki.

Kwenye ujumbe alioweka kwenye mitandao ya kijamii, Dkt Ruto aliambatanisha barua aliyowatumia maaskofu hao, akisema amekuwa tayari kushiriki mazungumzo bila masharti yoyote.

Kauli yake ilionekana kumwelekezea lawama Rais Kenyatta kama ndiye aliye kizingiti kikuu kwa mazungumzo hayo.

You can share this post!

Wanasiasa wasukuma ngome zao kujisajili

Amref yamtaka Uhuru aondoe kafyu