HabariSiasa

Ruto ampisha Raila

February 24th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

KWA mara kadhaa sasa, Naibu Rais William Ruto ameonekana kumpisha kinara wa upinzani Raila Odinga kuhutubu kabla ya Rais katika mikutano ya hadhara, hatua ambayo ni kinyume na itifaki rasmi.

Kimsingi, Bw Odinga anapaswa kuongea kabla ya Naibu Rais ambaye baadaye humualika Rais kutoa hotuba yake, lakini hali imekuwa tofauti katika siku za hivi punde, taswira ambayo imezua maswali mengi kuhusu nafasi ya Bw Odinga serikalini.

Wachanganuzi wa masuala ya uongozi wanasema hali hiyo inaonyesha kuimarika kwa uhusiano kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga tangu kutokea kwa ‘handisheki’ mnamo Machi 9, 2018.

Awali, Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa, walikuwa na uhasama mkubwa dhidi ya Bw Odinga wakisema kuwa lengo lake lilikuwa ni kusababisha vurugu katika chama cha Jubilee.

Kwa wakati mmoja, Dkt Ruto alinukuliwa akimlaumu Bw Odinga kwa kutaka kujiunga na serikali kupitia mlango wa nyuma na kudai kwamba alikuwa na njama ya kutaka afukuzwe katika chama cha Jubilee.

Hata hivyo, kuanzia mwaka huu, Dkt Ruto na washirika wamebadilisha kauli zao kuhusu muafaka kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta na kusifu juhudi za kuunganisha Wakenya.

Wamekuwa wakiandamana na Rais Kenyatta kuhudhuria hafla mbalimbali kote nchini ambako Dkt Ruto amekuwa akimpisha Bw Odinga kuzungumza na wananchi kabla ya kumkaribisha Rais kuhutubu.

Katika ziara ya Kaunti ya Kisii mapema wiki hii ambapo Rais alifungua hospitali ya rufaa, Dkt Ruto alimwalika Bw Odinga kuzungumza kabla ya kumwalika Rais Kenyatta kutoa hotuba yake.

Hali ilikuwa hivyo wakati Rais na Bw Odinga walipozuru Kisumu kuzindua mpango afya kwa wote (UHC) ambao ni mojawapo wa nguzo za maendeleo za serikali ya Jubilee.

Hafla nyingine, ambayo Dkt Ruto alimwalika Bw Odinga kuzungumza kabla ya Rais ni sherehe za Mashujaa Dei zilizofanyika mjini Kakamega, ngome nyingine ya Bw Odinga.

Katika Kongamano kuhusu Ufisadi mapema mwaka huu katika Ukumbi wa Bomas, Nairobi Bw Odinga alilazimika kukalia kiti cha Naibu Rais, akisubiri Dkt Ruto akamilishe hotuba yake.

“Kabla ya kukualika mheshimiwa Rais, ili kukuza na kuendeleza umoja wa kitaifa, niruhusu nimwalike Bw Odinga atoe hotuba yake kwanza,” alisema Dkt Ruto huku akimpisha Bw Odinga aliyekalia kiti chake, hali iliyozua kicheko.

Wakati wa sherehe za Madaraka Dei mnamo 2018 zilizofanyika katika uwanja wa Kinoru, Kaunti ya Meru, Dkt Ruto alimuomba Rais amruhusa ili amwalike Bw Odinga kuhutubu.

“Nakuomba ruhusa kwa heshima Mheshimiwa Rais nimwalike aliyekuwa Waziri Mkuu. Kwa sababu tuko katika msimu wa kuwaunganisha Wakenya, wacha nimualike Bw Odinga,”alisema Dkt Ruto.

Alipoanza kuhutubu, Bw Odinga alimtaja Naibu Rais kama rafiki na ndugu huku umma ukishangilia.

Mara ya mwisho ambapo Bw Odinga alipuuzwa hadharani na Bw Ruto ilikuwa katika sherehe za Madaraka Dei mnamo 2017 mjini Nyeri, wakati ambapo bado miungano ya Jubilee na NASA ilikuwa na uhasama mkubwa wa kisiasa.

Wadadisi wanasema Dkt Ruto hakuwa na budi kubadilisha mbinu zake baada ya kugundua kuwa hangefaulu kumpiga vita Bw Odinga baada ya kuanza kushirikiana na Rais Kenyatta.

“Dkt Ruto alitambua kwamba angepoteza umaarufu na hata kuaibika kwa kuendelea kumpuuza Bw Odinga na muafaka kati ya kiongozi huyo wa upinzani na mkubwa wake Rais Kenyatta,” alisema mdadisi wa masuala ya siasa Danstan Omari ambaye ni wakili.

“Dkt Ruto aligundua kwamba angetengwa na viongozi hao wawili katika ziara zao kote nchini na hivyo kubaki katika giza. Kumbuka Dkt Ruto ni mwanasiasa mpevu na ili kulinda nafasi yake serikalini, hawezi kukubali kukosa katika mikutano ambayo Rais na Bw Odinga wanahudhuria,” alisema Bw Omari. Kulingana na mdadisi mwingine wa siasa Thomas Maosa, Dkt Ruto aligundua kwamba alikuwa akijipiga vita mwenyewe na akaamua kujitosa katika meli ya muafaka shingo upande.

“Ni hali tu inayomfanya Dkt Ruto kumkumbatia Bw Odinga. Moyoni mwake anafahamu kwamba kumpuuza wakati akiwa na ukuruba wa kisiasa na Rais Kenyatta ni kupoteza,” alisema.

“Ukifuatilia kwa makini, kile ambacho Dkt Ruto anatambua zaidi katika ushirikiano wa Rais Kenyatta na Bw Odinga ni kuunganisha Wakenya kwa ajili ya maendeleo. Pili, huwezi kumdharau hadharani mtu ambaye ana ukuruba mkuu na mkubwa wako ambaye ni rais wa nchi,” alisema.