Habari

Ruto ampongeza Feisal Bader kwa kupata ushindi Msambweni

December 16th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto Jumatano asubuhi amempongeza mwandani wake Feisal Abdallah Bader kwa kushinda kiti cha ubunge cha Msambweni.

Bader, ambaye aliwania kama mgombeaji huru, alipata kura 15,251 na kumbwaga mgombeaji wa ODM Omari Boga ambaye alipata jumla ya kura 10,444 katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika Jumanne, Desemba 15, 2020.

“Pongezi rafiki yangu Feisal Bader. Ushindi wako ni thibitisho la imani kwa Mungu na kuaminiwa na watu. Demokrasia na nguvu za wananchi zimeshinda. Watu wa Msambweni Mungu awabariki. Pongezi E. Mwihaki (Gaturi), S. Waiganjo (Lake View), K. Ochieng (Kahawa Wendani) na washindi wengineo. Kwa waliopoteza, msubiri wakati mwingine,” Dkt Ruto akasema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Kiti cha ubunge cha Msambweni kilisalia wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge Suleiman Ramadhan Dori baada ya kuugua kansa, mnamo Machi 29, 2020.

Bader ni mpwawe marehemu Dori ambaye aliingia bungeni kwa tiketi ya chama cha ODM.

Baada ya kifo cha Dori, chama cha Jubilee, kupitia Katibu Mkuu Raphael Tuju, kilitangaza kuwa hakingedhamini mgombea katika uchaguzi mdogo na kuunga mkono mgombea wa ODM kwa “moyo wa handisheki”.

Hapo ndipo Dkt Ruto akamkaribisha Bader nyumbani kwake Karen na kutangaza kuwa atamuunga mkono kuwania kiti hicho kama mgombea wa kujitegemea.

Tangu wakati huo, wandani wa Dkt Ruto wamekita kambi Msambweni wakimpigia debe Bader wakiongozwa na Gavana wa Kwale Salim Mvurya.