Habari za Kitaifa

Ruto amrejesha Muthaura serikalini kwa kumteua chansela wa KU

January 20th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA Mkuu wa Utumishi wa Umma Balozi Francis Muthaura amerejea tena serikalini kufuatia uteuzi wa hivi punde uliofanywa na Rais William Ruto.

Bw Muthaura, 77, aliyehudumu chini ya marais wa zamani Daniel Moi, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, ametunukiwa wadhifa wa Chansela wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Kulingana na toleo la Januari 19 la Gazeti Rasmi la Serikali, balozi Muthaura atashikilia wadhifa huo kwa kipindi cha miaka mitano.

Uteuzi wa Bw Muthaura umesawiriwa kama hatua ya Rais Ruto ya kueleza nia yake ya kuwazawadi watu walioshtakiwa pamoja naye katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), The Hague, Uholanzi, 2012.

Mnamo Agosti 9, 2023 aliyekuwa mtangazaji wa redio ya Emoo FM Joshua Arap Sang’ aliteuliwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma katika Afisi ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei.

Bw Sang’ pia ni mmoja wa Wakenya sita walioshtakiwa pamoja na Rais Ruto katika ICC kwa makosa ya uhalifu wa kibinadamu kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Wengine ni Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, Waziri wa zamani na Mbunge wa Tinderet Henry Kosgei na aliyekuwa Kamishna wa Polisi Hussein Ali.

Sita hao walielekezewa tuhuma hizo na aliyekuwa Mwendesha Mashtaka Mkuu katika ICC Luis Moreno Ocampo.

Hata hivyo, mashtaka dhidi ya sita hao yaliondolewa, nyakati tofauti kuanzia 2013, kutokana na ukosefu wa ushahidi.

Wakati huo huo, Rais Ruto amemteua aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Katiba (CIC) Charles Nyachae kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Mafunzo ya Masuala ya Serikali (KSG).

Mwaka 2023, Nyachae alijiuzulu wadhifa wake wa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki kuhusu Haki (EACJ), nafasi aliyoteuliwa na rais wa zamani Bw Kenyatta.