Habari

Ruto amzidi Uhuru, Raila

September 13th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William anawashinda maarifa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga katika juhudi zao za kuzima umaarufu wake unaozidi kuongezeka nchini.

Wawili hao wanaunga marekebisho ya Katiba kupitia mchakato wa maridhiano (BBI) ambao Dkt Ruto anapinga.

Ingawa Rais Uhuru Kenyatta hajamtaja Dkt Ruto moja kwa moja kwenye matamshi yake ya kukashifu wanaokosoa BBI na vita dhidi ya ufisadi, wandani wake na wa Bw Odinga wamekuwa wakimtaka ajiuzulu kwa kupinga mageuzi ya Katiba wakidai anamkaidi Rais.

Wadadisi wanasema miito hii inalenga kumsukuma Dkt Ruto kumkabili mkubwa wake hadharani jambo ambalo amekwepa kabisa. Juzi wakati washirika wake walipotoa matamshi dhidi ya familia ya Rais Kenyatta, wanasiasa wanaounga handisheki walimtaka ajiuzulu wakidai ni yeye aliwatuma.

“Lakini Dkt Ruto aliwazidi maarifa na kujitenga na matamshi hayo akiwataka washirika wake wasimkosee heshima kiongozi wa nchi na familia yake. Kwa kufanya hivi aliwazima waliomhusisha na madai hayo na watu wakamuunga mkono wakidai alionyesha uongozi bora. Watu walimsifu wakisema ingawa wandani wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakitumia lugha isiyo na heshima dhidi yake, hawajawahi kuwaonya,” alisema mchanganuzi wa siasa Edward Kisiangani.

Wadadisi wanasema kwamba licha ya kutengwa katika chama cha Jubilee na serikalini huku wanasiasa na maafisa wa serikali wakitishwa wasimuunge mkono, umaarufu wake unazidi kuongezeka iliposhuhudiwa katika mikutano ya hivi punde Nairobi, Machakos na Kisii. Hii ni kwa sababu wakati Rais Kenyatta na Bw Odinga walipokuwa wakitumia maafisa wa serikali na vigogo wa kisiasa kumkata kucha, Dkt Ruto alibadilisha mbinu na kujenga mtandao wa viongozi wa mashinani kote nchini kupitia kampeni yake ya kusaidia masikini.

Duru zinasema Dkt Ruto amebuni kamati za vijana mashinani kote nchini. Hii imeimarisha umaarufu wake. Pia, ameunda kamati ya washauri wa kisiasa na viongozi wa kidini na wanaharakati wanaoweka mikakati ya kumpigia debe kote nchini.

Wakati washirika wake walipopokonywa nyadhifa za uongozi katika chama cha Jubilee, Dkt Ruto aliwataka waheshimu uamuzi wa Rais Kenyatta. Kwa kufanya hivi alizima juhudi za kumtaka amjibu Rais.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen anamtaja Dkt Ruto kama kiongozi mwerevu, mvumilivu na anayestahimili mawimbi mengi hatari kwa sababu ya mikakati thabiti ya kisiasa.

“Hakuna kiongozi anayeweza kuvumilia dharau na matusi kama Naibu Rais William Ruto. Hata hivyo, hiyo haimaanishi kwamba yeye ni mjinga,” asema Bw Murkomen.

Licha ya wandani wake kukamatwa na kuhangaishwa kwa kukosoa serikali, Dkt Ruto hajajitokeza hadharani kuwatetea hatua ambayo wandani wake wanasema imewakanganya wanaompiga vita.

Dkt Ruto amekuwa akibadilisha kila hatua na tamko linalonuiwa kumpiga vita kumfaidi.

Wakati Rais Kenyatta alipomlaumu kwa kutanga tanga, alibadilisha kauli hiyo kuwa vuguvugu la kisiasa ambalo limekuwa maarufu nchini.

Kulingana na Dkt Ruto nia yake ya kuzuru maeneo tofauti lilikuwa ni kukagua miradi ya maendeleo kufanikisha ajenda za serikali.

Hata hivyo, washirika wa Rais Kenyatta walimlaumu kwa kutumia ziara zake kupigia debe azima yake ya urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Rais Kenyatta alipomteua Waziri wa usalama wa ndani kusimamia utekelezaji wa miradi ya serikali, Dkt Ruto aligeuza mbinu na kuanza kutembelea makanisa kuchanga pesa hatua ambayo wadadisi wanasema imesaidia kuimarisha umaarufu wake kote nchini.

“Hata janga la corona halikumzuia Dkt Ruto kuendelea kukutana na viongozi wa kidini na mahsla. Amekuwa akikutana nao kuomba na kuwasaidia. Hata walipodai aligawa chakula chenye sumu hawakufaulu,” asema pasta mmoja jijini Nairobi ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Vile vile Waziri wa Mazingira alipomuita karani, Dkt Ruto alibadilisha kauli hiyo kumfaidi kwa kujiita karani wa mahasla. Licha ya wanasiasa kutishwa wajitenge naye, Dkt Ruto amewavuta waliokuwa mahasimu wake upande wake wakiwemo waliokuwa maseneta Boni Khalwale, Hassan Omar na Johnstone Muthama.