Ruto anyemelea ngome ya NASA

Ruto anyemelea ngome ya NASA

Na KAZUNGU SAMUEL na LUCAS BARASA

HATA kabla ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga kuzuru Pwani katika msururu wao wa mikutano ya kuhubiri umoja, Naibu Rais William Ruto ameonekana kutumia umoja wa viongozi hao, kunyemelea ngome za muungano wa NASA.

Kabla ya kuelekea Pwani Ijumaa ambapo alilakiwa kwa heshima na wabunge wa upinzani, Bw Ruto alifanya mikutano kadhaa na viongozi kutoka Kaunti ya Meru pamoja na wawakilishi wa kinamama wote nchini katika makao yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

Bw Ruto ambaye alikuwa Mombasa Ijumaa, Kwale Jumamosi na leo akitarajiwa Taita Taveta alilakiwa kwa heshima na wabunge wa upinzani ambao ni washirika wa karibu wa magavana Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi).

Gavana Kingi na Gavana Joho pia wameeleza azma yao ya kuwania Urais mwaka wa 2022.

Katika tukio ambalo wengi hawakuwa wakilitarajia kabla ya Raila Odinga na Rais Uhuru Kenyatta kushikana mikono, mapema mwezi huu, takribani wajumbe 20 kutoka eneo hilo ambao ni wanachama wa ODM walisema watafanya kazi pamoja na Bw ruto.

Na ili kuwavuta karibu wanasiasa hao, naibu huyo wa Rais alionekana akiweka keki ya maendeleo kama chambo huku akiwaambia wawe tayari kwa maendeleo lukuki kutoka kwa serikali ya Jubilee.

“Lazima sasa tushirikiane na wananchi kuendeleza taifa hili hasa baada ya Rais na Bw Odinga kuamua kushirikiana kuendeleza taifa baada ya muda mwingi wa kuchapa siasa,” akasema Bw Ruto.

“Siasa sasa ni lazima iwe historian a tuanze kuangalia masuala ya maendeleo. Miradi hii yote ambayo tunafanya ni kwa ajili ya kuwafanyia kazi wananchi kama tulivyoahidi.

Ukanda wa Pwani unajulikama kama ngome ya kisiasa na katika uchaguzi wa mwaka wa 2013, ulipigia kura Bw Odinga. Kisha kwa kuonyesha umahiri wake, Bw Raila aliwataka wakazi kugomea marudio ya uchaguzi wa mwezi Oktoba na wakamsikiliza.

Bw Odinga, amefanya vigumu kwa vigogo wa Jubilee kufanya kampeni zao Pwani ambayo imekuwa ikijikakamua kutoka kwa lindi la umaskini na kuachwa nyuma kimaendeleo.

Licha ya kuwa Pwani ndio ngome ya kiuchumi kutokana na uwepo wa bandari, na pia katika setka ya kitalii, kaunti zote sita za Pwani bado zinakumbana na baa la umaskini, ukosefu wa kazi, ukosefu wa miundo msingi.

Hakuna barabara nzuri, uhaba wa maji na tatizo la uskowta ambalo limektaa kabisa kumalizika.
Kaunti za Mombasa, Lamu, Kwale, Kilifi, Tana River na Taita Taveta ni ufunguo wa uchumi wa taifa hili hasa kutokana na mradi wa Lapsset huko kaunti ya Lamu.

Viongozi wakuu wa Pwani ambao ni Bw Kingi na Bw Joho wamekuwa wakisukuma siasa za kujitenga baada ya uchaguzi wa mwaka jana ambao ulikumbwa na utata.

 

You can share this post!

Aapa kuadhibu mume wake kwa kumchunguza kama ana mpango wa...

Baraza la Agikuyu lamtaka Raila aendelee kuikosoa serikali

adminleo