Ruto aonywa asifurahie masaibu ya Rais Uhuru

Ruto aonywa asifurahie masaibu ya Rais Uhuru

Na WAANDISHI WETU

Naibu Rais William Ruto na washirika wake wa kisiasa wanaendelea kusherehekea masaibu ya mkubwa wake Rais Uhuru Kenyatta kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ulioharamisha jaribio la kubadilisha katiba huku wandani wa Rais wakionya kuwa furaha yao ni ya muda mfupi tu.

Wandani wa Rais walianza vikao vya kubuni mikakati ya kukomboa mchakato huo muhimu kwa Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wanaosisitiza lengo lao ni kuunganisha Wakenya.

Dkt Ruto ambaye alipinga mchakato huo kwa dai la kutoshirikishwa kikamilifu aliwataka wakereketwa wa mpango huo kuheshimu uamuzi wa mahakama.

“Demokrasia yetu imekitwa katika utawala wa sheria, kuheshimu katiba, kutenganishwa kwa mamlaka ya tanzu za serikali na kuheshimu taasisi huru. Wakenya wote wazalendo wanafaa kulinda haya kama vile mahakama ilivyofanya,” alisema Dkt Ruto.

Akipuuza wanaotaka kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Dkt Ruto aliwataka kuzingatia upatikanaji wa chanjo ya virusi vya corona, ufufuzi wa uchumi, Ajenda Nne Kuu za maendeleo na kuunganisha nchi.

Dkt Ruto alisema hayo huku wandani wake wakiandaa sherehe maeneo tofauti kufurahia uamuzi wa kuzima BBI.Gavana wa Makueni, Prof Kivutha Kibwana, mmoja wa waliowasilisha kesi zilizosababisha mchakato huo kuzimwa, alisema kwamba uamuzi wa Mahakama ni baraka kwa Naibu Rais.

“Huenda mtu asimpende Naibu Rais William Ruto. Huenda mtu asiwe upande wake. Lakini kwa suala hili la BBI, historia itamhukumu vyema. Msimamo wake umethibitisha Katiba ya 2010 ambayo mwanzoni hakuitaka,” Gavana Kivutha alisema katika taarifa jana.

Katika Kaunti ya Kirinyaga, baadhi ya wakazi walifurahia uamuzi wa Mahakama Kuu wakitaja mchakato wa BBI kama matumizi mabaya ya pesa.

Naye mbunge wa Igembe Kusini, Kaunti ya Meru Paul Mwirigi alitaka uchunguzi kuhusu pesa zilizotumiwa katika BBI na waliohusika waagizwe kuzirudisha.

“Hata kama wakikata rufaa, hakutakuwa na refarenda isipokuwa waongeze muhula wao uongozini. Tumekuwa tukisisitiza kuwa mchakato huu ni haramu. Uchunguzi unafaa kufanywa na wale walioidhinisha pesa kutumiwa wazirudishe,” alisema Bw Mwirigi.

Diwani wa Wadi ya Municipality, Bw Elias Murega alisema mswada huo haukutimiza mahitaji ya kikatiba.Gavana wa Migori Okoth Obado na Seneta wa Kaunti hiyo, Bw Ochillo Ayacko walitofautiana kuhusu uamuzi huo.

Bw Obado aliusifu lakini Ayacko akaukosoa akisema ulichochewa na hisia za uanaharakati katika mahakama. Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Laikipia waliandamana kulalamikia uamuzi wa kuharamisha BBI.

Ripoti ya Benson Matheka, Pius Maundu, James Murimi, David Muchui, George Munene na Ian Byron

You can share this post!

DINI: Akili yako itawaliwe na mawazo mema usiwe adui wa...

MAYATIMA WA BBI