HabariSiasa

Ruto apokelewa kwa shangwe Mombasa

March 16th, 2018 1 min read

Na KAZUNGU SAMUEL

ZAIDI ya wabunge 10 kutoka mrengo wa NASA Ijumaa walimpokea kwa heshima Naibu Rais William Ruto alipohudhuria mkutano mkubwa katika eneo la Jomvu, Kaunti ya Mombasa.

Bw Ruto alikuwa katika eneo hilo la Jomvu kuanzisha ujenzi wa barabara ya Jomvu -Rabai.

Wabunge hao wakiongozwa na mwenyekiti wa wabunge wa Pwani Bw Suleiman Dori walisema kwa pamoja kuwa wataendelea kushirikiana na serikali kwa minajili ya maendeleo.

“Kwa sasa hivi tunachoangalia ni maendeleo na kwa sababu Baba na Rais wameamua kushirikiana, basi tunatarajia hili kuendelea huku pia. Sasa tuko pamoja kwa maendeleo,” akasema Bw Dori.

Mbunge wa Jomvu ambako ujenzi huo wa barabara utaanzia, Bw Badi Twalib alisema kuwa muafaka mpya kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Raila Odinga ni ishara njema.

‘Ushirikiano huu sasa ni mwamko mpya na ndio maana unaona tumekuja pamoja. Barabara hii itakuwa na faida nyingi kwetu kama wakazi wa Jomvu na viunga vyake,” akasema Bw Twalib.

Akihutubia wakazi, Bw Ruto alisema wakati wa siasa umeisha.

“Haya mambo ya siasa hayana nafasi. Wacha tuchape kazi. Vile Raila na Rais waliamua kushirikiana na kuendeleza maisha ya Wakenya mbele,” akasisitiza Ruto.