Habari

Ruto apokezwa noti mpya

June 7th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amepokea rasmi noti mpya iliyozinduliwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) katika hafla iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa maadhimisho ya Madaraka Dei katika uwanja wa michezo mjini Narok.

Dkt Ruto Alhamisi jioni alipokezwa noti ya nambari ya pili ya utambulisho (serial number) na Gavana Patrick Njoroge afisini mwake katika jumba la Harambee Annex, Nairobi.

Serikali kupitia CBK ilizundua noti hizo mpya wakati wa sherehe za Madaraka Dei katika hatua ya kutimiza hitaji la kikatiba.

Akiongea baada ya kupokea sarafu hizo, Naibu Rais alitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono CBK katika mchakato huo.

“Ninawahimiza wananchi wote kukumbatia noti hii mpya kwani imezinduliwa kuafiki Katiba na kurahisisha shughuli za kiuchumi,” akasema huku akiipongeza CBK kwa ‘kazi nzuri’.

Noti zote zina picha ya Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Jomo Kenyatta (KICC) lililoko Nairobi.

Pia zina picha za wanyamapori ambao wameiletea nchi hii sifa kwa kuwa kivutio cha watalii.

Dkt Njoroge alisema sarafu hizo mpya zimesanifiwa kufikia masharti yaliyowekwa na CBK, kuridhia matamanio ya umma na kuendana na hitaji la katiba.

Nyuma ya noti ya Sh50 kuna picha inayoashiria kawi safi (green energy) huku ile ya Sh100 ikiwa na picha zinazoonyesha shughuli za kilimo.

Noti ya Sh200 ina picha za kuonyesha huduma za kijamii, zile za Sh500 zina picha ya kuonyesha mandhari ya utalii na ile ya Sh1000 ina picha zenye mandhari ya shughuli ya utawala bora.

Noti hizo zimetengenezwa kwa njia ambapo zinaweza kutambuliwa kwa urahisi na watu wasio na uwezo wa kuona.

Uzinduzi wa noti mpya unajiri baada ya kuzinduliwa kwa sarafu mpya (coins) na Rais Kenyatta mnamo Desemba 2018 kulingana na hitaji la Katiba ya sasa.

Katiba hii ambayo ilizinduliwa mnamo Agosti 27, 2010, inasema kuwa sarafu na noti mpya zinafaa kuwa na picha zinazoonyesha utajiri na historia ya Kenya lakini hazifai kuwa na picha za mtu yeyote.