Habari MsetoSiasa

Ruto apuuza Jubilee na ODM kuungana

March 18th, 2019 1 min read

Na VITALIS KIMUTAI

NAIBU Rais Dkt William Ruto amesema chama cha Jubilee hakiwezi kuunda muungano wowote na ODM kinachoongozwa na Raila Odinga.

Dkt Ruto akizungumza wakati wa hafla ya kumkaribisha nyumbani Mbunge wa Ainamoi, Silvanus Maritim, alisema manifesto za vyama hivyo viwili hazioani na muungano wowote kati yao hauwezi kutimia kwa sasa au siku zijazo.

“Tunasikia watu wa ODM wanataka kuandaa mazungumzo ili kuunganisha chama chao na chetu. Sisi hatuna muda wa kuketi na mabroka wa kisiasa, waenezaji wa propaganda na walaghai. Washughulikie kazi yao kwenye upinzani na waachane na sisi,” akasema Dkt Ruto.

Vile vile alimwonya Bw Odinga dhidi ya kuendelea kusambaratisha miradi ya serikali, na badala yake akamtaka kuwaelekeza wabunge wake kumakinikia kazi za upinzani katika Mabunge ya Kitaifa na ya Seneti.

“Ni wazi mbele ya umma kuwa Bw Odinga alivunja NDP, Narc, CORD, NASA na sasa amegeukia Jubilee. Hatutamruhusu kuvunja chama chetu kamwe,” akasema.

“Nawaomba wafuasi wa Jubilee kukaa chonjo na kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni zinatimia kabla ya uchaguzi mkuu ujao. Sisi tuna deni la kuwajibikia wananchi na lazima tuafikie hilo,” akaongeza Dkt Ruto.

Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, aliyeandamana na Dkt Ruto kwenye hafla hiyo, alimhakikishia kuwa wapiga kura wa eneo la Mlima Kenya wako nyuma yake na kumtaka apuuze madai kwamba wamemtoroka kutokana na salamu za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

“Nataka kumhakikishia Naibu Rais kwamba watu wa Mlima Kenya wako nyuma yake na watampigia kura kwa wingi kutokana na jinsi alivyotufaa hapo nyuma. Pia ningependa kuweka wazi kwamba Rais Kenyatta hajamtoroka Dkt Ruto jinsi inavyodaiwa,” akasema Bw Waititu.

Bw Odinga na Dkt Ruto wamekuwa wakikabiliana vikali katika siku za majuzi kuhusu masuala mbalimbali.