Habari Mseto

Ruto ararua BBI

October 27th, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto alijipata mpweke katika ukumbi wa Bomas kwa kukosoa mapendekezo ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) ambayo ilizinduliwa Oktoba 26, 2020.

Ingawa viongozi wengi waliohudhuria kongamano la jana waliunga mkono mapendekezo hayo na kuahidi kuhamasisha umma yapitishwe kwenye kura ya maamuzi na bungeni, Dkt Ruto alisema hajashawishika kuwa yatatimiza malengo ya kuunganisha Wakenya.

Akizingumza mbele ya Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake katika mchakato huo Raila Odinga, Dkt Ruto alikosoa mapendekezo ya kubadilisha Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), pendekezo la kubuni wadhifa wa afisa wa kupokea malalamishi katika Idara ya Mahakama atakayeteuliwa na rais na hatua za kupokonya Seneti jukumu la kuamua mgao kwa kaunti.

Pia alikosoa pendekezo la kubuniwa kwa Baraza la Polisi litakalosimamiwa na waziri wa usalama wa ndani na hatua ya kubuni nyadhifa za waziri mkuu na manaibu wake.

Alionya dhidi ya kuunga mkono baadhi ya mapendekezo, akisema yanaweza kutumiwa kuwadhulumu wale wanaoyashinikiza.

Dkt Ruto alitaja hatua ya kubuni wadhifa wa afisa wa kupokea malalamishi kuhusu mahakama kama itakayopokonya idara hiyo uhuru wake na kuifanya ithibitiwe na serikali kuu. Alieleza kuwa mahakama inafaa kutengewa pesa zaidi kujenga korti nchini ili kuimarisha utoaji wa haki kwa Wakenya.

UHURU WA MAHAKAMA

“Kuna juhudi za kuhujumu uhuru wa mahakama. Kurejesha Kenya katika enzi ambazo majaji walikuwa wakipigiwa simu na maafisa wakuu kupatiwa maagizo jinsi ya kufanya kazi yao ni hatari,” alisema Dkt Ruto.

Ripoti ya BBI inapendekeza kuwa rais ateue afisa atakayekuwa kamishna wa Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kupokea malalamishi kuhusu utendakazi wa majaji na mahakama kwa jumla.

Kulingana na Dkt Ruto, mageuzi yanayohitajika katika mahakama ni kuipatia pesa za kutosha kujenga mahakama kote nchini na kuajiri majaji zaidi. Alionekana kumlenga Rais Kenyatta ambaye amekataa kuteua majaji 41 waliopendekezwa na JSC.

Huku akizomwa na waliohudhuria kongamano hilo kwa kukosoa mapendekezo ya ripoti hiyo, Dkt Ruto alisema kwamba hajashawishika kuwa kubuni wadhifa wa waziri mkuu na manaibu wake wawili kutamaliza tatizo la ubaguzi katika uwakilishi katika serikali kuu.

“Naomba kushawishiwa jinsi kuwa na nyadhifa hizi kutaimarisha ushirikishi kwa sababu ni rahisi kwa nafasi hizo kutwaliwa na watu kutoka chama kimoja cha kisiasa kitakachoshinda uchaguzi,” alisema.

USHIRIKISHI

Alitoa mfano wa chama tawala cha Jubilee, ambacho kwa kuwa kina idadi kubwa ya wabunge, kinashikilia nyadhifa za viongozi wa wengi katika bunge na seneti: “Kwa heshima zote naomba kuelezewa hali ikiwa hivi, vinara wenza wa muungano wa upinzani kama NASA wataenda wapi,” alihoji.

Katika mapendekezo yake, BBI inasema kubuniwa kwa nyadhifa za waziri mkuu, manaibu wake wawili, kiongozi rasmi wa upinzani bungeni na kuteua mawaziri miongoni mwa wabunge kutahakikisha Wakenya wote watashirikishwa katika serikali ya kitaifa. Lakini Dkt Ruto alitilia shaka utekelezaji wa pendekezo hilo akisema sio tiba ya hulka ya mshindi wa uchaguzi kutwaa vyeo vyote vikuu.

Dkt Ruto alisema pendekezo kwamba vyama vya kisiasa viteue makamishna wa IEBC litapokonya tume hiyo uhuru wake wa kuandaa uchaguzi huru na wa haki. Alifananisha hatua hiyo na soka ambapo baadhi ya timu zinateua mwamuzi wa mechi: “Mimi ni mwanasayansi na sio mwanasoka kama Bw Odinga. Kwa sababu anaelewa masuala ya soka, naomba anieleze ikiwa katika hali hii, ligi inaweza kuwa ya haki kweli?” alihoji.

Kuhusu pendekezo la kupokonya Seneti jukumu la kugawa pesa kwa kaunti na kuongeza idadi ya maseneta wanawake, Dkt Ruto alisema ni sawa na kudhalilisha ugatuzi na kuwadharau wanawake. “Unawezaje kuongeza idadi ya wanawake katika Seneti ambayo haina nguvu za kuamua masuala ya kaunti,” aliuliza wajumbe ambao walikuwa wakimzoma.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress Musalia Mudavadi na Gavana wa Kitui Charity Ngilu, pia walikosoa pendekezo la kupokonya Seneti jukumu la kuamua pesa kwa kaunti. Bi Ngilu na Mudavadi walisema Seneti inafaa kuwa na mamlaka zaidi kuliko bunge.

Kulingana na Mudavadi, afisa wa kupokea malalamishi kuhusu mahakama na majaji, anafaa kuteuliwa na Jaji Mkuu wala sio rais.

Tofauti na Dkt Ruto ambaye alisema hajashawishika kuunga ripoti hiyo, Bw Mudavadi na Bi Ngilu walisema wataipigia debe ipite katika kura ya maamuzi.

Dkt Ruto alisema BBI inafaa kushirikishwa kwenye mdahalo wa kitaifa kwa uwazi ili kila mmoja aridhike kabla ya kura ya maamuzi.

KUCHOCHEA ‘UHASLA’

Wakati huo huo, vinara wa siasa waliohutubu jana walimlaumu Naibu Rais William Ruto kwa madai ya kuchochea uadui kati ya matajiri na maskini.

Walisema kwamba kuna hatari ya kuzuka kwa vita vya kitabaka ikiwa ataendelea kufanya hivyo.

Ingawa hawakumtaja kwa jina, waliozungumza walisema kuwa kauli za baadhi ya wanasiasa zimekuwa zikigonganisha Wakenya.

“Mheshimiwa rais, ninataka kuwaambia viongozi, baadhi ambao wameketi nawe katika jukwaa kuu waache kuzua vita vya matabaka kupitia miradi yao,” alisema Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio ambaye ni kiongozi wa wengi katika Seneti.

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alisema baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwachochea makundi ya watu dhidi ya mengine kupitia vuguvugu la hasla.

Kiongozi wa Chama cha Mashinani Isaac Ruto alisema baada ya kusoma ripoti hiyo aligundua haina njama fiche baadhi ya wanasiasa wanaoipinga wanavyodai.

Alisema ataifanyia kampeni ipitishwe kwenye kura ya maamuzi kwa vile imeongeza pesa kwa kaunti kwa kuzitengea asilimia 35 ya mapato ya serikali.

“Iletwe tuipitishe ilivyo na isikawie,” alisema. Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula alisema ripoti hiyo inahakikishia Wakenya amani, matumaini na ustawi. “Tumekuwa tukishuhudia machafuko kila baada ya uchaguzi. Hii ripoti inawapa Wakenya matumaini makubwa na maendeleo,” alisema.

Katibu Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi nchini (Cotu) Francis Atwoli, alipendekeza muungano huo uruhusiwe kuteua mbunge kuwakilisha maslahi ya wafanyakazi. Viongozi wa vijana, wawekezaji na akina mama pia waliahidi kupitisha ripoti hiyo.