Habari MsetoSiasa

Ruto arejea Kiambu akisema katumwa na Rais

June 2nd, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

SIKU chache baada ya kikundi cha wanasiasa kumpiga Naibu Rais William Ruto marufuku kukanyaga Kaunti ya Kiambu, Dkt Ruto Jumapili alirejea kaunti hiyo kifua mbele, akisema alienda kwa idhini ya Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe.

Akizungumza alipofika katika kanisa moja mtaa wa Kahawa Wendani, eneobunge la Ruiru, Naibu Rais alisema alikuwa amemfahamisha Rais Kenyatta kuwa angefika eneo hilo, na hata Rais akampa ‘barua’ amfikishie.

Hii ilikuwa takriban wiki moja tu baada ya baadhi ya wanasiasa wanaompinga kutoka eneo la Mlima Kenya kumkanya kufika Kiambu, bila kuandamana na Rais.

“Nawaletea salamu nyingi sana kutoka kwa kiongozi wetu wa taifa, mheshimiwa Uhuru Kenyatta. Asubuhi ya leo nilikuwa naye, amesafiri kwenda kazini kule Canada, ameondoka asubuhi ya leo na akanituma salamu nyingi,” Dkt Ruto akasema katika kanisa hilo.

“Nilimwambia nilikuwa na mpango wa kuja katika kanisa hili la Askofu Waweru na akanituma hata na barua ya kanisa hili ndio tuweze kuendelea mbele,” Naibu Rais akaendelea.

Maneno yak yalikuja baada ya baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo ambao walikuwa wameandamana naye kuwakashifu waliotoa vitisho hivyo kwa Dkt Ruto, wakisema hawana usemi wowote.

Naibu Rais alikuwa ameandamana na viongozi kadhaa, wakiwamo wa Kiambu Kimani Ichungwa (Kikuyu), Simon Kingara (Ruiru), Gabriel Kago (Githunguri), Githua Wamacukuru (Kabete), Jude Njomo (Kiambu ya kati) na Jonah Mburu (Lari).