Habari Mseto

Ruto arejea nchini baada ya ziara ya Dubai

November 23rd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto alirejea nchini Jumapili bila mbwembwe zozote baada ya kukamilisha ziara ya siku nne jijini Dubai, katika Milki za Kiarabu (UAE).

Mbunge mmoja ambaye ni mwandani wake wa karibu Jumatatu aneambia Taifa Leo kwamba ndege iliyombeba kiongozi huyo iliwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) mwendo wa saa nne asubuhi.

“Ni kweli, bosi alirejea jana saa nne mchana. Lakini sidhani kwamba hiyo ni stori kwa sababu yuko salama na buheri wa afya. Wale ambao wamekuwa wakiendesha uongo mitandaoni kuhusu ziara yake ni watu ambao hawana kazi ya maana ya kufanya,” akasema mbunge huyo kutoka eneo la North Rift ambaye aliomba tulibane jina lake.

Habari kuhusu ziara ya Dkt Ruto ilithibitishwa Ijumaa alipoweka picha na video mitandaoni ambapo alionekana pamoja na mpishi na mfanyabiashara maarufu Nusrek Gokche, anayejulikana ulimwenguni kwa jina, “Salt Bae”.

Kwenye video moja Naibu Rais alionekana akikatiwa nyama na mfanyabiashara huyo, raia wa Uturuki, katika mojawapo ya mikahawa yake (Salt Bae).

Dkt Ruto pia alichapisha picha zilizomwonyesha akikutana na Makamu wa Rais wa zamani wa Nigeria Atiku Abubakar na mwanaharakati wa kisiasa nchini Nigeria, Timi Frank.