Habari za Kitaifa

Ruto aridhishwa na usambazaji fatalaiza licha ya ‘soko’ kusheheni mbolea feki  

April 9th, 2024 2 min read

NA WAANDISHI WETU 

RAIS William Ruto ameelezea kuridhishwa kwake na shughuli ya usambazaji mbolea ya ruzuku hata baada ya Wizara ya Kilimo kuthibitisha kuwa baadhi ya mbolea hizo ni feki na kuagiza zisiuziwe wakulima.

Wizara iliagiza uchunguzi ufanywe kuhusu sakata hiyo huku ikiahidi kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wamiliki wa kampuni zinazouza mbolea hizo feki.

Hata hivyo, jana, Jumatatu, Aprili 8, 2024 Rais Ruto aliagiza kuwa mbolea hiyo isambazwe haraka ili ifaidi wakulima wakati huu ambapo mvua imeanza kunyesha kwa wingi kote nchini.

Kiongozi wa taifa alisema hayo alipotembelea bohari la Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao, mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu.

“Tunapunguza bei ya pembejeo za kilimo ili tuweze kupambana na njaa,” Rais Ruto akasema.

Alitoa onyo kali kwa wahusika katika sakata ya uuzaji wa mbolea feki akisema wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Dkt Ruto alisema kuwa serikali yake itaendelea kupunguza bei ya mbolea ili kuifanya shughuli ya kilimo iwe yenye faida.

“Hata hivyo, hatutaki kutoa manufaa hii kwa kilimo cha mahindi pekee. Tunapanua mimea yetu ili kuongeza mapato yetu,” akaongeza.

Rais Ruto alisema kuwa taifa hili linaweza kuendeleza sekta ya kiviwanda kupitia kilimo cha malighali yatakayotumika katika viwanda hivyo.

Wiki jana, serikali kupitia Wizara ya Kilimo ilisimamisha uuzaji wa mbolea zinazotengenezwa na kampuni ya KEL Chemicals, iliyoko Thika, Kaunti ya Kiambu.

Hii ni baada ya uchunguzi kubaini kuwa mbolea yake aina ya N.P.K 10.26.10 haijatimiza viwango hitajika vya ubora.

Baada ya kuzimwa kwa uuzaji wa mbolea hiyo, Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (Kebs) ilichukua hatua ya kisheria dhidi ya wamiliki wa kampuni hiyo kwa kuuza mbolea hiyo kinyume na Sheria kuhusu Viwango Sura ya 496.

“Hatua hii inaonyesha kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa wakulima wanauziwa pembejeo ambazo zinatimiza viwango vya ubora ili kulinda sekta ya kulimo,” ikaeleza taarifa hiyo kutoka kwa Wizara ya Kilimo.

Taarifa hiyo iliwahakikishia wakulima kuwa mbolea zote zinazosambazwa chini ya mpango wa uuzaji mbolea ya ruzuku zimetimiza viwango hitajika vya ubora isipokuwa mbolea inayotengenezwa na kuuzwa na kampuni ya KEL Chemicals.

Miongoni mwa mbolea inayouzwa na kampuni hiyo lakini haijatimiza viwango hitajika vya ubora ni pamoja na Kelphos Plus, Kelphos gold na NPK 10:26:10.

Wakati huo huo, Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo inapendekeza kuwa wakulima walionunua mbolea feki kutoka kwa mabohari ya NCPB walipwe fidia.

Uongozi wa kamati hiyo ulilalamika kuwa mamia ya wakulima walipata hasara kubwa na hivyo wanafaa kusaidiwa.

“Wakulima walitumia pesa nyingi kununua mbolea ambayo hawajatumia kwa sababu ni feki. Kwa hivyo, serikali inafaa kuwarejeshea wakulima pesa zao ili wanunue mbolea halisi wakati huu wa msimu wa upanzi,” mwenyekiti wa kamati hiyo Kamau Murango akasema.

Taarifa ya STANLEY KIMUGE, BARNABAS BII na GEORGE MUNENE