HabariSiasa

RUTO ARUDI NYANZA TENA

November 8th, 2018 2 min read

VIVERE NANDIEMO na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto hapo Jumamosi atarejea tena katika Kaunti ya Migori, siku nne tu baada ziara yake iliyosusiwa na wabunge wa chama cha ODM katika kila kinachotajwa kama mbinu ya kupenya ngome ya ODM kwa ajili ya uchaguzi wa 2022.

Bw Ruto atatembela eneobunge la Kuria Mashariki ambako atafungua chuo cha kiufundi kilichoko eneo la Kendege na kuongoza harambee ya kuchangia makanisa zaidi ya 20.

Kulingana na mbunge wa eneo hilo, Marwa Maisori Kitayama, anayeshirikisha ziara hiyo, Bw Ruto atatembelea eneo hilo kutimiza ahadi yake ya kufungua rasmi chuo hicho na kusaidia makanisa kukusanya pesa.

“Mipango ya kumkaribisha Naibu Rais eneo la Kuria imekamilika. Ziara yake ni ya kutimiza ahadi aliyotoa alipotembelea eneo hilo miezi miwili iliyopita. Wakati huu atakuja kufungua chuo cha Kiufundi cha Kendege, na kuongoza harambee ya makanisa ya hapa,” alisema Bw Kitayama.

Hata hivyo, alisema Bw Ruto hatazindua ujenzi wa barabara ya Isibania-Kehancha-Kegonga-Ntimaru.

“Naibu Rais aliomba kuzinduliwa kwa ujenzi wa barabara hiyo kuairishwe hadi mwaka ujao kwa sababu atakuwa na shughuli mahali pengine na hatapata wakati,” alieleza mbunge huyo.

Migori ni ngome ya chama cha ODM cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga japo eneo la Kuria lilipigia kura wabunge wa Jubilee kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Bw Ruto, anayemezea mate urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, amekuwa akijaribu kupenya ngome cha Bw Odinga.

Mnamo Jumatatu, alitembelea eneo la Suna Magharibi ambapo alizindua ujenzi wa barabara ya Muhuru-Suna-Kehancha na mradi wa stima katika mji wa Masara.

Hata hivyo, ziara hiyo ilikosolewa na wabunge wa ODM waliodai hakuwakushirikisha wakisema lengo lake ni kujipigia debe katika azima yake ya kugombea urais 2022.

Viongozi wa ODM wa kaunti hiyo akiwemo Seneta Ochillo Ayacko hawakuandamana naye. Alikaribishwa na gavana Okoth Obado pekee, aliyekuwa mbunge wa Nyatike Edick Anyanga na wabunge kutoka Kuria Mathias Robi (Kuria Mashariki) na Kitayama.

Mbunge wa Nyatike Tom Odege, ambaye anawakilisha eneo alilotembelea Bw Ruto alipuuza ziara hiyo akisema ni ya kuharibu wakati. Alimlaumu Bw Ruto akisema anazindua miradi ambayo haijatengewa pesa.

“Alikuja hapa kujaribu bahati yake kisiasa kwa kuzindua miradi hewa ambayo haijatengewa pesa kwa sababu kama mwanachama wa kamati ya bunge kuhusu miundomsingi, ninawaambia barabara hii haijatengewa pesa,” alisema Bw Odege.

Mwenyekiti wa chama cha ODM, John Mbadi ambaye ni mbunge wa Suba Mashariki alisema Bw Ruto hakuwashirikisha wabunge wanaohudumu mbali aliwaalika wale wa zamani.

Naye mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, alimlaumu Bw Ruto kwa kutumia muafaka wa Rais Kenyatta na Bw Odinga kuvamia ngome za chama chao mada,i ambayo Naibu Rais alipuuza akisema analipwa kuhudumia Wakenya na kutembelea maeneo yote nchini.

Bw Kitayama alitetea ziara za Ruto eneo hilo na kuwalaumu wanasiasa wa ODM kwa kucheza siasa badala ya maendeleo.