Habari Mseto

Ruto asema endapo atakosa tiketi 2022 atamuunga mkono mwaniaji wa JP

May 23rd, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais William Ruto amesisitiza kwamba ikitokea hapati tiketi ya kuwania urais katika Jubilee Party basi ataunga mkono yeyote atakayeteuliwa kuwania urais 2022 kwa tiketi ya chama hicho tawala.

Dkt Ruto pia amewataka watakaokuwa washindani wake kumuunga mkono ikiwa atateuliwa kuwania kiti hicho.

Mapema Alhamisi kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Kameme, Naibu Rais amesema kuwa Jubilee ni chama cha kitaifa kinachothamini demokrasia.

“Atakayeteuliwa kuwania kiti cha urais nitamuunga mkono. La muhimu ni kwamba iwapo Wakenya wataamua nipeperushe bendera, basi ninawasihi wenzangu waniunge pia,” akasema Dkt Ruto.

Amesema Jubilee, chama tawala kwa sasa na kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, kitakubali kuwa katika mrengo wa upinzani endapo kitarambishwa sakafu katika uchaguzi mkuu.

“Kushindwa sio mwisho, asiyekubali kushindwa si mshindani,” amesema.

Kauli ya Ruto inajiri wakati ambapo Jubilee inaonekana kugawanyika kwa mirengo miwili; mrengo ambao viongozi wake wanasema wanaridhia kwa dhati salamu za maridhiano baina ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM  Raila Odinga na ule unaomuunga mkono Naibu Rais.

Siasa chafu

Wakati wa mahojiano na kituo hicho, Dkt Ruto amesema wakosoaji wake wanaendesha siasa ambazo zinaenda kinyume na matakwa ya Jubilee ya kufanya maendeleo.

“Hizo ni siasa tu, zisizo na mwelekeo. Jubilee lazima iafikie ajenda zake za maendeleo kwa wananchi,” akasema.

Baadhi ya wakosoaji wake wamekuwa wakimsuta kulemaza jitihada za Rais dhidi ya ufisadi na hata kutilia shaka michango yake ya mara kwa mara makanisani..

Ameendelea kueleza kwamba yuko katika mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi.

Pia, amepinga vikali kwamba amekuwa akitetea washukiwa wanaotajwa katika sakata za ufisadi.