Ruto asusia Kongamano la Ugatuzi

Ruto asusia Kongamano la Ugatuzi

Na WAANDISHI WETU

NAIBU RAIS William Ruto jana alisusia Kongamano la Saba la Ugatuzi lililoandaliwa katika Kaunti ya Makueni licha ya kuratibiwa kama mgeni wa heshima aliyefaa kulifunga rasmi.

Dkt Ruto ambaye aliendelea na misururu ya mikutano ya kujipigia debe katika Kaunti ya Nyandarua, badala yake alimtuma Mkuu wa Wafanyakazi katika afisi yake jambo ambalo lilikataliwa na magavana waliohudhuria kongamano hilo.Baada ya kukataa na kupuuza ujumbe wa Dkt Ruto wakiona kama kitendo cha dharau kwa kongamano hilo kubwa, magavana hao walimgeukia Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa ambaye alihutubu na kulifunga rasmi.

“Tulikuwa tumetarajia Naibu Rais ahudhurie na kufunga kongamano hili. Hata hivyo, mwenyekiti wa baraza letu Martin Wambora aliniarifu kuwa Dkt Ruto alimpigia simu usiku na kusema kuwa atamtuma mkuu wa wafanyakazi kwenye afisi yake kusoma ujumbe wake,” akasema Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya.

“Kama magavana, hili ni kongamano la kimataifa na si mtu yeyote anaweza kufika hapa na kutoa hotuba,” akaongeza. Kabla ya kongamano la mwaka huu ambalo ni la saba, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akihutubu siku ya ufunguzi wake huku Kinara wa ODM Raila Odinga akitoa hotuba siku ya pili naye Dkt Ruto amekuwa akifika siku ya tatu na kulifunga rasmi.

Katika makala ya mwaka huu, Rais Kenyatta na Bw Odinga, wote walihutubu siku ya kwanza huku Jaji Mkuu Martha Koome akitoa hotuba yake kwa wajumbe waliohudhuria siku ya pili.Dalili kuwa Naibu Rais hangehudhuria kongamano hilo ilianza kuonekana mapema baada ya Waziri wa Ugatuzi Charles Keter kuhepa baada ya kuonekana tu kwa muda mchache siku ya ufunguzi.

Bw Keter, mwandani wa Dkt Ruto aliondoka na kuenda zake baada ya hotuba ya Rais siku ya kwanza na hakuonekana tena Makueni. Siku hiyo aliondoka hata kabla ya Bw Odinga na Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i kutoa hotuba zao.Akiwa katika Kaunti ya Nyandarua, Dkt Ruto aliwataka wakazi wa Mlima Kenya ‘warudishe’ mkono kwa kuwa amemuunga mkono Rais Kenyatta mara mbili (2013 na 2017).

Alihutubia mikutano katika vituo vya kibiashara vya Ndogino, Mairo Inya, Ndaragwa na Kwa Kung’u ambapo alishikilia kuwa ndiye mwaniaji bora zaidi anayetosha kurithi kiti cha Urais kutoka kwa Rais Kenyatta 2022.“Dawa ya deni ni kulipa. Tulikubaliana na Rais kuwa tutaongoza nchi hii kwa miaka 20 ili tutekeleze miradi mingi ya maendeleo.

Ajenda yetu ya kuendeleza nchi hata hivyo ilipigwa breki na maridhiano kupitia ‘handisheki’,” akasema Dkt Ruto. Alikuwa ameandamana na wabunge Rigathi Gachagua (Mathira) Alice Wahome (Kandara), Senators John Kinyua (Laikipia), Kithure Kindiki (Tharaka Nithi) miongoni mwa wanasiasa wengine.

Wakati huo huo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru, amemkashifu Dkt Ruto kwa kumtaka Jaji Mkuu Martha Karua aondoke kwenye kamati inayoratibu uchaguzi mkuu ujao.“Hawa ndio watu ambao walituambia kuwa hata ukimweka Dkt Oburu Oginga (Mbunge wa EALA na kakake Bw Odinga) mwenyekiti wa IEBC bado watashinda kura.

Ni nini imebadilika kiasi kwamba sasa wameingiwa na uoga na wanaeneza madai yasiyokuwa na msing?’’ akauliza Mucheru.

You can share this post!

TAHARIRI: Aina mpya ya Covid ikabiliwe isilete lockdown

WANDERI KAMAU: Wakati wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko...

T L