RUTO ATIKISA ODM: Wabunge wa ODM waapa kumuunga Ruto 2022

RUTO ATIKISA ODM: Wabunge wa ODM waapa kumuunga Ruto 2022

CHARLES WASONGA na MOHAMED AHMED

NAIBU Rais William Ruto ameyumbisha chama cha ODM hasa Pwani baada ya viongozi sugu wa chama hicho kinachoongozwa na Raila Odinga kukaidi maagizo yake na kuendelea kuunga mkono azma ya Bw Ruto kuongoza Kenya 2022.

Hii ni baada ya Bw Ruto katika ziara zake Pwani kuyeyusha nyoyo za viongozi wa kanda hiyo akiwemo Gavana Amason Kingi wa Kilifi, ambaye mwaka 2017 alikuwa mkosoaji mkubwa wa Naibu Rais na Rais Uhuru Kenyatta.

Pia wabunge kadhaa waliochaguliwa kwa tiketi ya ODM wamejitokeza hadharani kusimama na Bw Ruto kwenye ndoto yake ya kuwa rais.

Kinachoshangaza zaidi ni viongozi hao kukaidi maagizo ya ofisi kuu ya ODM. Wakiongozwa na Bw Kingi, viongozi hao wamepuuzilia mbali vitisho vya ODM kuwa itaaadhibu wanachama ambao wametangaza kumuunga mkono Bw Ruto.

Jumatano iliyopita Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alionya kuwa chama hicho kitaadhibu wanachama ambao wametangaza kumuunga mkono Naibu Rais kugombea urais.

Alisema wanachama hao wamekiuka makubaliano na mwongozo wa chama na hivyo wanastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Bw Kingi, ambaye ni mmoja wa vigogo wa siasa Pwani, alisema hatua ya viongozi wa eneo hilo kumkumbatia Bw Ruto imetokana na muafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

“Lengo la mwafaka lilikuwa ni kuponya na kuleta umoja wa nchi, kutuliza taharuki ya kisiasa na kutuwezesha kufanya kazi na wapinzani wetu. Ninaomba Naibu Rais azidi kuendelea kututembelea mara nyingi iwezekanavyo. Tunafanya kile ambacho Raila alifanya na hatutarudi nyuma,” akasema.

Akizungumza katika Hoteli ya Sai Eden Roc mjini Malindi wakati wa futari na harambee ambayo pia ilihudhuriwa na Bw Ruto, gavana huyo alisema juhudi za kuleta umoja wa Pwani zimeanza kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Naye Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa alisema Bw Ruto pekee ndiye mgombeaji urais anayeweza kuungwa mkono 2022.

Wabunge Suleiman Dori (Msambweni), Badi Twalib (Jomvu) na Benjamin Tayari (Kinango) nao pia wametangaza kumwunga mkono Bw Ruto.

Bw Dori alisema ifikapo 2022, eneo hilo lazima liwe ndani ya serikali na hilo litawezekana tu kama watamuunga mkono Bw Ruto.

Kwa upande wake, Bw Tayari ameshikilia kuwa watamuunga mkono Naibu Rais ili kuhakikisha Serikali ya Jubilee inaendelea kutekeleza ajenda yake ya maendeleo.

Wabunge hao pia walikosoa msimamo wa ODM kuwa wataadhibiwa huku Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya akisema maamuzi ya chama hayawezi kupewa uzito kuliko Katiba inayowapa Wakenya haki ya kujieleza.

 

Sifuna hana la kufanya

“Bw Sifuna amekosa kazi ya kufanya. Inafaa atuache tufanye kazi yetu. Hatuwezi kunyamazishwa na maamuzi ya chama. Bw Ruto ni mshirika katika muafaka wa kuleta umoja na ataendelea kuwa katika mijadala yetu,” akasema Bw Baya.

Bw Twalib naye alisisitiza kuwa mazungumzo ya umoja yalianzishwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga ili kuwezesha watu kushirikiana na viongozi wa vyama vyote ndiposa wakaamua kumwunga mkono Bw Ruto.

“Kiongozi wa chama chetu alisema muafaka hauhusu 2022 ndiposa tumemchagua Bw Ruto kwa sababu tunajua yeye ndiye atatuongoza siku zitakazofuata 2022. Kama Bw Ruto amedhihirisha kuwa ana uwezo unaotufaa tutazidi kumuunga mkono,” akasema akiongeza kuwa watapambana na hatua za kinidhamu jinsi zitakavyokuja.

Katika hotuba yake, Bw Ruto aliwashutumu wakazi wa Pwani kwa kumtafuta kila mara wanapohitaji misaada ilhali ikifika wakati wa uchaguzi hawamtaki.

Alishangaa kwa nini wakazi wengi wa eneo hilo huunga mkono upande wa upinzani ambao hushindwa uchaguzini na haujawahi kuwasaidia kujenga barabara, madaraja na shule.

 

Mbona vigeugeu?

“Ninawauliza kwa nini ifikapo wakati wa kazi na harambee za kuboresha maisha, kujenga shule na makanisa mwanitafuta lakini mbona wakati wa uchaguzi mnatafuta mtu mwingine?” akauliza.

Katika uchaguzi wa mwaka uliopita, kaunti hiyo haikuchagua kiongozi yeyote wa Jubilee ikiwemo katika wadhifa wa madiwani licha ya viongozi wa chama hicho kukita kambi kwa muda mrefu wakipiga kampeni na kuzindua miradi ya maendeleo.

“Wapwani saa zingine inafaa muwe na huruma. Jameni hata kiti cha udiwani mlikataa kunipa licha ya yale mazuri na ziara zote nilizofanya Pwani! Nitawashtaki kwa Mungu,” akasema kwa utani.

Kuhusu ufisadi, Bw Ruto alionya viongozi wanaojaribu kuingiza siasa katika juhudi za kupambana nao na kusema vita dhidi ya ufisadi ni ajenda ya serikali na haibagui upande wowote wa kisiasa.

Alisema hayo baada ya ripoti kutokea kuwa baadhi ya wanasiasa wa Rift Valley wanaamini juhudi zinazoendelezwa kupambana na ufisadi zinalenga wandani wake.

Jumapili aliendeleza ziara katika maeneo mbalimbali ya Pwani ambapo alitoa ahadi za mamilioni ya pesa za maendeleo huku akitafuta uungwaji mkono.

You can share this post!

Mwanamke ashangaza korti kusamehe madume 5 waliombaka

Ajabu ya baba mzazi kumlawiti mwanawe ulevini kisha kumpa...

adminleo