HabariSiasa

Ruto atumia Facebook kupeperusha hotuba ya Raila

July 15th, 2019 1 min read

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto, Jumatatu aliduwaza Wakenya alipopeperusha video ya moja kwa moja ya hotuba ya hasimu wake mkubwa wa kisiasa, Bw Raila Odinga katika mtandao wa kijamii wa Facebook.

Wawili hao walikuwa miongoni mwa wageni wakuu katika ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya biashara katika jumba la KICC jijini Nairobi.

Hafla hiyo ilisimamiwa na Waziri wa Biashara na Viwanda, Bw Peter Munya, ambaye ni mmoja wa mawaziri waliodaiwa kupanga njama ya kumuua Naibu Rais.

Bw Odinga alisema anazungumza kama balozi wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU).

Alitaja masuala kama vile ufisadi, urasimu na uchochezi wa kisiasa kama changamoto kuu zinazotatiza biashara kati ya mataifa ya bara hili.

Alikashifu Tume ya Kudhibiti Kawi na Petroli kwa kuhangaisha waekezaji wanaotaka kufanya biashara ya kuzalisha kawi nchini, ambayo ni rasilimali muhimu ya kuvutia viwanda.

“Hii nchi inahitaji uzalishaji wa kawi zaidi. Hakuna mwekezaji wa viwanda vikubwa atakuja hapa akiona kiwango tunachozalisha cha kawi kinatoshana na kile tunachotumia,” akasema.

Kwa upande wake, Dkt Ruto alisema alihudhuria kikao hicho baada ya kuombwa kufanya hivyo na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa na shughuli zingine.

Alitilia mkazo umuhimu wa Kenya kuimarisha uwezo wa kuuza bidhaa zake nje ya nchi na wafanyabiashara wakome kulalamikia ukosefu wa soko, bali wajikakamue kuingia katika masoko yaliyopo.

Kulingana naye, serikali za kaunti zina jukumu muhimu kuchangia katika uzalishaji wa bidhaa zinazoweza kusafirishwa nje ya nchi baada ya kutengenezwa viwandani.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Wycliffe Oparanya, wawakilishi wa mabalozi wa nchi za kigeni na waekezaji wa kibinafsi.