Siasa

Ruto aunganisha wawaniaji wa kiti kukabili ODM Msambweni

October 12th, 2020 2 min read

Na MOHAMED AHMED

NAIBU Rais William Ruto amewaunganisha wawaniaji wa kiti cha ubunge cha Msambweni nyuma ya Feisal Bader, ili kumkabili mwaniaji wa chama cha ODM, Omar Boga.

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto alikutana na Peter Nzuki, Bashir Kilalo na Bakari Sebe, ambao waliamua kuweka kando mipango yao ya kuwania kiti hicho, na badala yake kumuunga mkono Bw Bader.

“Ni furaha kuona kuja pamoja kwa wawaniaji wa kiti cha Msambweni ambao wameamua kumuunga mkono mgombeaji huru Feisal Bader,” akasema Dkt Ruto kupitia mitandao yake ya kijamii.

Dkt Ruto alikutana na wafuasi wa mashinani wa wawaniaji hao katika afisi yake ya Nairobi, ambao walikuwa wameandamana na wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), George Theuri (Embakasi West), Nixon Korir (Lang’ata) na waliokuwa maseneta Hassan Omar (Mombasa) na Johnstone Muthama (Machakos).

Bw Kilalo ambaye alikuwa awanie kiti hicho kupitia tiketi ya ANC, aliingia chama cha Kadu Asili na baadaye kuingia kambi ya Dkt Ruto na kumuunga mkono Bw Bader.

Bw Nzuki wa chama cha Democratic Party aliunga mkono upande wa Bw Ruto na kuwaacha Bw Khamisi Mwakaonje wa UGM na Abdulrahman Shee wa Wiper pamoja na Sharlet Mariam kumenyana na Bw Boga wa ODM.

Kuwaleta pamoja viongozi hao kulijiri siku moja tu baada ya kikosi cha Dkt Ruto kuzuiliwa kufanya mkutano eneo la Kwale ambao ulikuwa unalenga kutekeleza suala hilo la kuungwa mkono kwa Bw Bader.

Huku Dkt Ruto akionekana kuweka mipango yake kwa ajili ya Bw Bader, Bw Boga kupitia chama chake cha ODM ameeleza kuwa wana imani watashinda uchaguzi huo.

Mwenyekiti wa ODM tawi la Kwale, Hassan Mwanyoha, aliambia Taifa Leo kuwa tayari wameshikilia kura za mashinani licha ya kuwa hawajaanza kampeni rasmi.

“Wao wameanza kukusanya nguvu zote pamoja lakini sisi tunawaambia kuwa hilo halitutishi. Hata wakiwa wamechukua asilimia 10 sisi tunasema ile asilimia kubwa ambayo ni 90 yote tunayo sisi,” akasema Bw Mwanyoha.

Alisema kwa sasa wameanza kampeni za chini kwa chini wakisubiri kufanya mkutano karibuni.

Aliongeza kuwa maafisa wa chama watakutana ili kuweka mipango yao kwa ajili ya uchaguzi huo wa Disemba 15.