Habari

Ruto avamia ngome ya Raila

July 14th, 2020 2 min read

JUSTUS OCHIENG NA WANDERI KAMAU

KAMBI ya kisiasa ya Naibu Rais William Ruto imeanza kuvamia eneo la Nyanza kujaribu kushawishi wakazi hasa vijana kumuunga mkono.

Mnamo wikendi, washirika wawili wakuu wa Dkt Ruto, Ndindi Nyoro (Mbunge wa Kiharu) na Oscar Sudi (Mbunge wa Kapseret), walifanya ziara eneo la Bondo ambako ni nyumbani kwa Raila na Kisumu ambako walikutana na viongozi wa vijana.

Duru zilisema nia ya wawili hao ilikuwa ni kuwashawishi vijana kushiriki harakati za kumpigia debe Dkt Ruto mashinani katika eneo hilo ambako Bw Odinga anaungwa mkono kwa wingi.

Habari za kuaminika zilieleza kuwa pia kuna mpango wa kutuma ujumbe kutoka eneo la Luo Nyanza kwenda kumtembelea Naibu Rais nyumbani kwake Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu mara marufuku ya mikutano ya hadhara itakapoondolewa.

Tangu 2018 Dkt Ruto amekuwa akifanya juhudi za kujiimarisha katika maeneo yote ya nchi isipokuwa Luo Nyanza.

Taifa Leo imefahamu kuwa mpango wa kundi hilo unalenga kupenya eneo hilo kupitia makundi ya vijana, akina mama na makanisa.

HANDISHEKI

Pia wanaeneza ujumbe kuwa handisheki ilikusudiwa kutuliza nchi mbali sio kumpatia Bw Odinga urais hapo 2022.

“Kusudi la handisheki ni kumwezesha Rais Kenyatta kutawala kwa utulivu. Msitarajie atasema ‘Raila tosha’. Ahadi yake ilikuwa amalize miaka yake 10 ya utawala na kumpisha Ruto kuendelea,” akasema Bw Nyoro.

Mnamo Jumapili, Bw Sudi alikutana na kundi la vijana katika Ufuo wa Dunga wakiongozwa na Stephen Midenyo na aliyekuwa waziri wa biashara katika Kaunti ya Kisumu Richard Ogendo

Naye Bw George Ayugi alisema wako makini kumpigia debe Dkt Ruto eneo la Nyanza: “Hatuachi eneo lolote nje. Ingawa ODM ina ushawishi mkubwa Nyanza, mtaona mabadiliko. Hili ni eneo la ‘mahasla’ na tutawavuta wengi kwa Dkt Ruto.”

Waliokuwa maseneta, Johnston Muthama (Machakos) na Bony Khalwale nao waliambia Taifa Leo kuwa wanafanya kila juhudi kuhakikisha ushawishi wa Dkt Ruto umesambaa kila pembe ya nchi.

“Kuna kambi mbili za kisiasa nchini moja ikiongozwa na Uhuru, Raila na Gideon Moi na nyingine ni ya Ruto na Wakenya,” akasema Bw Muthama.

MATIBABU

Kwingineko, Bw Odinga alirejea nchini kimyakimya Jumapili usiku kutoka Dubai alikokuwa akipokea matibabu.

Kiongozi huyo aliondoka nchini siku chache kabla ya Juni 30, ambapo yeye na Rais Uhuru Kenyatta walitarajiwa kupokea rasmi ripoti ya jopo la BBI.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatatu, maafisa wakuu katika chama cha ODM walisema ingawa Bw Odinga anafahamu shauku walio nayo wafuasi wake kuhusu hali yake kiafya, atapumzika kwa siku kadhaa.

Jakom atapumzika kwanza ili kupata nafuu kiafya. Atatoa taarifa rasmi kwa Wakenya na wafuasi wake kuhusu masuala yote muhimu yanayoihusu nchi,” akasema Mkurugenzi wa Mawasiliano wa ODM, Philip Etale.

Ni kauli ambayo pia ilitolewa na msemaji wa Bw Odinga, Bw Dennis Onyango.

Ingawa wawili hao hawakueleza kwa kina masuala atakayogusia, Bw Odinga anarejea wakati ambapo kumekuwa na hali ya taharuki kati ya vyama vya ODM na Jubilee kuhusu ujumuishaji wa baadhi ya majina ya wabunge kwenye kamati muhimu za Bunge la Kitaifa.

ODM imekuwa ikilalamikia kujumuishwa kwa baadhi ya wabunge wa Jubilee kwenye kamati hizo, ikisema kuwa wengi wao wamekuwa wakipinga BBI.