Habari Mseto

Ruto avitaka vyuo vifunze kozi zinazowiana na Ajenda Nne Kuu

October 25th, 2018 1 min read

CHARLES WANYORO na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ametangaza kuwa kuanzia Ijumaa vyuo vikuu vitakuwa vikipokea ufadhili wa serikali kwa misingi ya ubunifu, utafiti na ubora wa watihimu kutoka vyuo hivyo.

Alisema hatua hiyo inalenga kuvihimiza vyuo hivyo kufundisha kozi ambazo zinaendana na mahitaji ya kimaendeleo nchini, haswa zile za kiufundi.

Bw Ruto alisema Alhamisi kwamba serikali imekuwa ikipunguza ufadhili kwa vyuo vikuu, kwa kutumia idadi ya wanafunzi kama kigezo pamoja na kozi ambazo zinafundishwa.

Akiongea katika Chuo Kikuu cha Embu wakati wa kuzinduliwa kwa Hazina ya Usaidizi chuoni humo, naibu rais alisema serikali inahitaji vyuo vikuu kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza utafiti na ubunifu kwa lengo la kuzalisha wafanyakazi wabunifu na wajasirimali.

“Serikali imeweka vyuo vikuu katika nguzo za ubunifu ili viweze kuisaidia kufanikisha ajende nne kuu za maendeleo kando na ustawi wa kiviwanda. Hii ndio maana kuanzia sasa tunataka vyuo vinavyofundisha kozi zinazoweza kutusaidia kutumiza lengo hilo,” akasema Bw Ruto.

Alivishauri vyuo vikuu kuanzisha kuegemea kozi za kiufundi ambazo alisema vina uwezo wa kuchochea maendeleo nchini.

“Vyuo vikuu vinapaswa kuzalisha wahitimu ambao watakuwa wa manufaa kwa uchumi wa taifa. Hatufadhili vyuo vikuu ambavyo wahitimu wao wataishia kuchoma mahindi kando mwa barabara za miji. Sharti vihakikisha kuwa wanafunzi wao wanapata ajira ili wachangia ukuaji na ustawi wa nchi.” Bw Ruto akasisitiza.

Kuhusu mitihani, naibu rais alisisitiza haja ya wahusika kuipa kipaumbele uwezo na umilisi wa wanafunzi wala sio lengo la kupita mitihani hiyo pekee.

“Hatupasi kuwashinikiza watoto wetu kupita mitihani pekee. Badala yake tunapaswa kuwahimiza kuwa weledi katika yale wanayofundishwa. Mfumo wetu wa kutumia mitihani kama kigezo cha kubaini ubora wa wanafunzi umepelekea wengi wao wenye talanta zingine kukoseshwa nafasi ya kujistawisha,” akasema.