Ruto avuliwa GSU

Ruto avuliwa GSU

LEONARD ONYANGO na ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto amemtaka Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai ampe maelezo kufuatia hatua yake ya kuondoa maafisa wa GSU nyumbani kwake katika mtaa wa Karen, Nairobi.

Makazi ya Dkt Ruto sasa yatalindwa na maafisa wa Polisi wa Utawala (AP) kutoka Kitengo cha Kulinda Majengo ya Serikali (SGB).

Maafisa wa SGB waliwasili nyumbani kwa Dkt Ruto wakiwa wameabiri magari mawili, wakazungushwa kila mahali na kuanza kutekeleza majukumu yao.

Msemaji wa Polisi Bruno Shioso, hata hivyo alisema kuwa mabadiliko hayo ni ya kawaida ndani ya kikosi cha polisi.

Kwamba Naibu wa Rais ataendelea kupewa ulinzi.

“Maafisa wa kusindikiza rais wataendelea kumpa ulinzi wa hali ya juu Naibu wa Rais,” akasema Bw Shioso.

Katibu wa Mawasiliano katika afisi ya Naibu wa Rais, David Mugonyi, Alhamisi alisema kuwa mkuu wa usalama katika makazi ya Naibu wa Rais mtaani Karen, alipigiwa simu na kufahamishwa kwamba maafisa wa GSU walifaa kuondoka kufikia saa nane mchana.

Bw Mugonyi alisema maafisa wa GSU walirejea kwenye makao yao makuu eneo la Ruaraka, ambapo wanangojea kupangiwa majukumu mengine.

“Ofisi ya Naibu wa Rais imemwandikia barua Inspekta Jenerali ili atoe maelezo kwa nini anahatarisha usalama wa Dkt Ruto kwa kumuondolea walinzi. Siasa hazifai kuingizwa katika suala la usalama wa Naibu wa Rais,” akasema Bw Mugonyi.

Hatua hiyo imejiri siku tatu baada ya Rais Uhuru Kenyatta, mnamo Jumatatu, kumtaka Dkt Ruto ajiuzulu ikiwa hajaridhika kuwa serikalini.

Siku moja baadaye, Dkt Ruto alipokuwa katika Kaunti ya Kwale, alimjibu kwa kusema kuwa hatajiuzulu.

Aliapa kuendelea kuwa afisini hadi ‘siku ya mwisho’.

Hatua hiyo ya serikali inakinzana na Kanuni za Utendakazi wa Huduma za Polisi.

Na kijijini nyumbani kwa Dkt Ruto katika eneo la Sugoi, Kaunti ya Uasin Gishu, vijana walijazana nje ya lango la Naibu wa Rais baada ya mabadiliko ya ulinzi kufanywa.

Maafisa wa GSU ambao wamekuwa wakilinda makazi ya Dkt Ruto ya Sugoi tangu 2013, waliondolewa na mahala pao kuchukuliwa na maafisa watatu wa AP.

Vijana hao waliipa serikali saa 24 kurejesha maafisa wa GSU la sivyo wayalinde wao wenyewe.

Sura ya 8 kuhusu majukumu ya GSU inasema kuwa maafisa wa kitengo hicho wanafaa kulinda Rais, Naibu wa Rais, Ikulu na Ikulu ndogo.

Maafisa wa GSU pia wana jukumu la kulinda baadhi ya kampuni za ndege za kigeni, kukabiliana na waandamanaji, kukabiliana na maharamia wa wanyamapori, wezi wa mifugo, magaidi na shughuli nyinginezo watakazoelekezwa na Inspekta Jenerali wa Polisi.

Alhamisi, Bw Mugonyi aliorodhesha visa ambapo ‘maafisa wa usalama wametumiwa kuhangaisha Naibu wa Rais’.

“Septemba 2020, maafisa wa polisi waliokuwa na silaha walizuia Naibu wa Rais kufanya mkutano katika Kaunti ya Kisii. Oktoba 2020, maafisa wa polisi walimzuia kwenda kanisani kwa ajili ya ibada katika Kaunti ya Murang’a,” akasema Bw Mugonyi.

Kuondolewa kwa GSU nyumbani kwa Naibu wa Rais Alhamisi kulizua hisia mseto huku wandani wake wakidai kuwa hatua hiyo inalenga kumshurutisha kujiuzulu.

Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja alikuwa miongoni mwa viongozi walioshutumu hatua hiyo ya Inspekta Jenerali wa Polisi Mutyambai.

“Naibu wa Rais ana haki ya kisheria kupewa usalama na wala suala hilo halina mjadala. Wakenya ndio walimchagua Dkt Ruto kuwa Naibu wa Rais. Wanaojaribu kumpokonya Dkt Ruto maafisa wa usalama wanamjenga kisiasa badala ya kummaliza. Akipokonywa walinzi Wakenya watamlinda. Nawasihi Bw Mutyambai, Waziri wa Usalama Fred Matiang’i na Katibu wa Wizara ya Usalama Karanja Kibicho kukoma kuingiza siasa katika suala la usalama. La sivyo wajiuzulu wajiunge nasi,” akasema Bw Sakaja.

You can share this post!

Gor Mahia yawasaka wavamizi 3 nje ya nchi

KIKOLEZO: Wameamua kukaa ngumu!