Habari za Kitaifa

Ruto awakausha madaktari KMPDU ikiapa kuendeleza mgomo

April 7th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

RAIS William Ruto amepuuzilia mbali matakwa ya madaktari nchini, huku akiwataka kusahau nyongeza ya mishahara wanayotaka.

Kulingana na kiongozi wan chi, Serikali haina pesa na kwamba madaktari wanapaswa kuishi hali ilivyo badala ya kulazimika ‘mambo ambayo hayatawezekana’.

Rais Ruto, hata hivyo, ameahidi kwamba serikali yake itaajiri wanafunzi madaktari wapatao 1, 500 wanaofanya mafunzo ya ziada.

Akizungumza Jumapili, Aprili 7, 2024 katika kanisa la Eldoret AIC Fellowship baada ya kuhudhuria ibada kimyakimya, Dkt Ruto alikiri kwamba anajua hali inayokabili madaktari na akawasihi wakubali kuishi kulingana na uwezo wa nchi ulivyo kwa sasa.

“Ninajua hali inayokabili madaktari na wahudumu wetu wa afya kwa jumla lakini ninataka kuwasihi kwamba ni muhimu kwetu kama taifa kukubaliana kwamba lazima tuishi kulingana na uwezo wetu,” alisema Rais Ruto.

Rais Ruto alisema kuwa nchi haiko tayari kutumia pesa ambazo hazipatikani kuashiria kuwa matakwa ya madaktari ya nyongeza ya mishahara hayatatekelezwa hivi karibuni.

Akizungumza kwa utulivu Ruto, hata hivyo, alisema hivi karibuni nchi itaandaa kongamano kujadili suala nzima la mishahara nchini.

“Hatuwezi kuendelea kutumia fedha ambazo hatuna, kwa kweli mambo mawili ya msingi sana yatatokea muda si mrefu, tutakuwa na kongamano kati ya Aprili 15 hadi 17 kujadili mishahara yetu kama taifa kwa sababu tunatumia Sh1.1 trilioni kulipa mishahara na ujira kutoka kwa Sh2.2 trilioni tunazokusanya kila mwaka kama mapato,” akasema.

Rais alisema kuna haja ya kurekebisha hali hiyo ikibainika kuwa nchi inatumia asilimia 47 ya mapato ya kila mwaka kwenye mishahara, badala ya asilimia 35 kama inavyotakikana kisheria.

“Tunahitaji mazungumzo ili tupunguze mzigo wa mishahara yetu kwa ajili ya maendeleo ili tukomboe rasilimali nyingi zaidi kwa kubuni ajira kwa vijana, kuhakikisha kwamba tunaweza kufadhili elimu yetu, afya na maendeleo kwa ujumla na hayo ndiyo mazungumzo ambayo lazima tuwe nayo,” akasema Rais Ruto.

Aidha, alifichua kuwa serikali itapunguza bajeti ya kila mwaka kutoka Sh4.2 trilioni hadi Sh3.7 trilioni ili kuishi kulingana na uwezo wa nchi.

“Lazima tuambiane ukweli, hatuwezi kuendelea kukopa pesa za kulipa mishahara. Ni sharti tuishi kwa mujibu wa uwezo wetu na ninaambia marafiki zetu madaktari tunawathamini na tunawajali, tunathamini kazi wanayofanya, huduma wanazotoa kwa taifa letu lakini lazima tuishi kulingana na uwezo wetu,” akasisitiza Rais Ruto.

Alisema rasilimali zilizopo zinatosha kulipa madaktari wanafunzi Sh70, 000 kwa mwezi kama malipo ya mwaka mmoja ujao kabla ya kuajiriwa.

Rais alihakikishia madaktari wanafunzi kuwa wote watapata nafasi katika hospitlai za umma.

“Tutachukua zaidi ya madaktari wanafunzi 1,500 na kuwalipa posho ya Sh70, 000 kwa mwezi tunapopanga kuwaajiri rasilimali zitakapopatikana,” alisema Bw Ruto.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari Nchini (KMPDU) Davji Atellah ameishutumu serikali kwa kuingiza siasa katika masuala ya afya.

“Serikali inacheza siasa na mambo mazito ya kiafya yanayoathiri Wakenya. Makataa ya siku 29 tulizotoa kwa serikali zilitosha kushughulikia malalamishi yetu, ukimya huu unamaanisha kwamba hawajali,” alisema Dkt Atellah alipozuru madaktari mjini Elodret wiki jana.

Viongozi wa KMPDU ambao walizuru mji wa Elodret maajuzi walisisitiza kwamba mgomo wa madaktari utaendelea hadi pale matakwa yao yatatimizwa.

“Tutaendelea na mgomo hadi serikali itimize matakwa yetu yote 19 kama ilivyo kwenye ilani ya mgomo ambayo tulitoa kwa serikali yapata mwezi mmoja uliopita,” alisema Dkt Atellah.

Dkt Atellah alipinga tetesi kuwa serikali imetekeleza baadhi ya matakwa yao.

“Hakuna takwa hata moja kati ya matakwa yetu 19 ambalo serikali imetekeleza,” alisema Dkt Atellah.