Ruto awaondolea lawama polisi waliovuruga mikutano yake

Ruto awaondolea lawama polisi waliovuruga mikutano yake

RUTH MBULA na WANDERI KAMAU

NAIBU Rais William Ruto, jana aliwaondolea lawama polisi waliovunja mikutano yake wiki iliyopita, na badala yake akalaumu wanaowapa maagizo ya kufanya hivyo.

Akizungumza akiwa Kaunti ya Nyamira ambapo polisi waliovunja mkutano wake walidumisha usalama, Dkt Ruto alisema polisi wanaelewa matatizo ya Wakenya.

“Polisi wetu hawana shida yoyote hata kidogo. Wanapitia changamoto kama Wakenya wengine. Wanaelewa matatizo yanayowakumba watu wetu,” akasema.

Jumanne iliyopita, Dkt Ruto alilazimika kukatiza mikutano miwili katika eneo hilo baada ya polisi kuifutilia mbali, wakisema hawakuwa wamejulishwa.

Hili lilifuatia kanuni zilizopitishwa na Kamati ya Kitaifa la Ushauri wa Usalama (NSAC) wiki iliyopita kwamba yeyote anayepanga kufanya mkutano lazima awajulishe polisi katika eneo husika angaa siku tatu kabla ya mkutano huo.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakimlaumu Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Katibu wa Wizara hiyo Karanja Kibicho kwa ubaguzi katika utekelezaji wa masharti hayo.

Kwenye mkutano huo, aliwakosoa vikali viongozi aliowalaumu kwa kuendesha siasa za kikabila.

“Mnapowasikia viongozi wakirejelea semi kama ‘kwetu’ ama ‘kwao’, lazima mjue kwamba hao ni wachochezi wa kikabila. Enzi za siasa kama hizo zimepita,” akasema.

Vile vile, aliwarai vijana kutokubali kutumiwa na baadhi ya viongozi kujihusisha kwenye ghasia.

Alieleza kuwa badala yake, wanapaswa kuwaunga mkono viongozi ambao wanawahusisha kwenye masuala ya maendeleo.

“Waambieni wale wanaowatumia kushiriki ghasia kuwaleta watoto na wake zao kuongoza shughuli kama hizo lakini sio nyinyi,” akasema.

Baadhi ya viongozi walioandamana naye ni wabunge Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Joash Nyamoko (Mugirango Kaskazini), Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi) na Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi.

Wabunge hao walisema kuwa hakuna vitisho vyovyote vitakavyowafanya kuacha kuunga mkono mikakati ya kuwasaidia vijana inayoendeshwa na Dkt Ruto.

Walitaja sekta ya bodaboda kuwa muhimu sana kwa ukuaji wa nchi, kwani imewaajiri mamilioni ya vijana.

Bw Osoro aliwakosoa polisi dhidi ya mapendeleo kwenye utekelezaji wa sheria.

You can share this post!

Moto walamba bweni nzima Shule ya Upili ya Musingu

Mvurya aunga mkono mgombeaji wa Ruto Msambweni